1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Jumuiya ya nchi za kiarabu yataka Israel iamuriwe kuondoa wanajeshi wake Lebanon

9 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDNM

Ujumbe wa jumuiya ya nchi za kiarabu, umelitolea mwito baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuiamuru Israel iwaondoe wanajeshi wake kutoka Lebanon kama sehemu ya kufikia makubaliano na kundi la Hezbollah.

Ufaransa na Marekani zimependekeza azimio la Umoja wa Mataifa linalonuia kuumaliza mgogoro wa Lebanon, lakini azimio hilo haliitishi Israel kuondoka Lebanon mara moja. Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Dan Gillerman, ametaka hatua kabambe zichukuliwe dhidi ya magaidi wa Hezbollah.

Gillerman pia amesema ipo haja ya kuwepo mkakati wa kimataifa wa kuzizuia Syria na Iran kuwapelekea silaha wanamgambo wa Hezbollah.

Hatua ya jumuiya ya nchi za kiarabu kulipinga azimio lililopendekezwa na Ufaransa na Marekani imeichelewesha kura iliyokuwa ipigwe juu ya azimio hilo, huku miito ya kutaka mapigano yasitishwe ikizidi kuongezeka.