1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu asimamishwa kizimbani katika kesi ya ufisadi

10 Desemba 2024

Waandamanaji wanao mpinga na wanaomuunga mkono Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamekusanyika nje ya mahakama ya mjini Tel Aviv wakati kiongozi huyo anasimama kizimbani kujibu tuhuma za ufisadi

https://p.dw.com/p/4nx14
Israel |Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Mahakamani mjini Tel AvivPicha: Menahem Kahana/REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesimamishwa kizimbani kuhusiana na kesi ya muda mrefu ya madai ya ufisadi, lakini pia makosa mengine yanayomkabili yanahusu kuanzisha tamasha la wiki nzima jambo ambalo linachukuliwa kama hatua ya kuchochea hisia za watu kwa lengo la kufunika masaibu ya kisheria yanayomkabili.

Soma Pia: Netanyahu akosoa uamuzi wa ICJ ni 'uamuzi wa uwongo 

Yote hayo yanajiri wakati ambapo Netanyahu anakabiliwa pia na hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake kwa makosa ya uhalifu wa kivita na wakati huo huo mashambulizi ya jeshi la Israel yakiwa yanaendelea katika Ukanda wa Gaza.

Israel |Mahakamani | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa Mahakamani mjini Tel AvivPicha: Menahem Kahana/REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amejaribu mara kwa mara kuchelewesha kufikishwa kwake mahakamani. Ni mara ya kwanza kwa waziri mkuu wa Israel kusimamishwa kizimbani akikabiliwa na makosa ya jinai, ni hatua ya kufedhehesha kwa kiongozi ambaye mara zote amekuwa akiweka taswira ya kuwa yeye ni mwanasiasa makini, mahiri na kiongozi wa kuheshimika.

Netanyahu atajibu mahakamani mashtaka ya udanganyifu, kuvunja uaminifu na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti zinazomkabili.

Soma Pia:  ICC yakabiliwa na shinikizo kufuatia waranti inazotoa

Anatuhumiwa kwa kupokea maelfu ya dola za Kimarekani, sigara na mvinyo wa bei ghali aina ya 'champagne' kutoka kwa bilionea mmoja mtayarishaji wa filamu wa Hollywood kwa makubaliano kwamba Netanyahu angelimsaidia katika mambo ya kibinafsi na ya kibiashara. Si hayo tu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, anakabiliwa pia na mashtaka yanayohusiana na kuendeleza udhibiti unaowanufaisha mabwanyenye wa vyombo vya Habari kwa makubaliano kwamba magwiji hao watampa Netanyahu nafasi ya juu kwenye vyombo vya habari pamoja na familia yake.

Netanyahu, aliye na umri wa miaka 75, anakanusha kufanya makosa, akisema mashtaka hayo ni njama ya kumchafua kisiasa inayoendeshwa na vyombo vya habari vinavyompinga na pia mfumo wa kisheria wenye upendeleo unaolenga kuupindua utawala wake uliodumu kwa muda mrefu. 

Hatua ya kiongozi huyo kusimama kizimbani kutoa ushahidi inafanyika baada ya Netanyahu na familia yake kukabiliwa kwa miaka mingi ya kashfa hizo.

Umati wa watu umekusanyika nje ya mahakama ya mjini Tel Aviv, wakiwa ni wafuasi wake na wale wanaompinga Netanyahu, wakiwemo wanafamilia wa mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa usalama wa Israel Itamar Ben-Gvir ni miongoni mwa waandamanaji wanaomuunga mkono Benjamin Netanyahu.

Israel Tel Aviv | Maandamano
Waandamanaji mjini Tel AvivPicha: Amir Levy/Getty Images

Mashtaka dhidi ya Netanyahu yamezusha mgawanyiko mkubwa nchini Israel, huku waandamanaji wakimtaka ajiuzulu na baadhi ya washirika wake wa zamani wa kisiasa wakikataa kuhudumu kwenye serikali ya kiongozi huyo wa Israel na kusababisha mzozo wa kisiasa ambao ndio chanzo cha kufanyika chaguzi tano nchini Israel katika muda wa chini ya miaka minne kuanzia mwaka 2019.

Soma Pia: Israel yasitisha vita Lebanon na kuendelea kuishambulia Gaza 

Benjamin Netanyahu ndiye waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel, akiwa ameshika wadhifa huo kuanzia mwaka 1996 hadi 1999, kisha mwaka 2009 hadi mwaka 2021, na kuanzia Novemba 2022 na kuendelea hadi sasa.

Vyanzo: AFP/RTRE