1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu apata ushindi mkubwa wa chama cha Likud

27 Desemba 2019

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepata ushindi mkubwa katika kinyang'anyiro cha kuwania uongozi wa chama tawala cha Likud. Ushindi huo unampa nguvu zaidi kiongozi huyo ambaye anakabiliwa na kashfa za ufisadi.

https://p.dw.com/p/3VNgd
Israel | Benjamin Netanjahu
Picha: picture-alliance/dpa/Photoshot

Haya yanajiri wakati ambapo kunatarajiwa kuandaliwa uchaguzi wa tatu wa nchi hiyo katika chini ya mwaka mmoja.

Baada ya kura zote kuhesabiwa, Netanyahu alipata ushindi wa asilimia 72.5 huku mpinzani wake Gideon Saar akipata asilimia 27.5. Saar alikiri kushindwa kwa kuandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema baada ya kura hiyo sasa atamuunga mkono Netanyahu katika uchaguzi mkuu uliopangiwa kufanyika mwezi Machi.

Netanyahu ambaye ndiye waziri mkuu aliyehudumu kwa kipindi kirefu zaidi nchini Israel alitarajiwa kumshinda mpinzani wake huyo, ingawa tofauti kubwa ya kura aliyomshinda nayo inaonesha kwamba nguvu yake imezidi katika nafasi anayoishikilia kwenye chama hicho ambacho amekiongoza kwa zaidi ya miaka ishirini.

Ushindi wa Netanyahu haumaanishi chochote kwa uchaguzi mkuu wa Machi

Hii leo, waziri mkuu huyo ameandika katika mtandao wa Twitter akiwapongeza wanachama wa Likud kwa kumpa ushindi huo na kudai kwamba atakiongoza chama hicho kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.

Israel | Gideon Saar
Gideon Saar, aliyekuwa mpinzani wa Netanyahu Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Wafuasi wake wamefurahishwa sana na ushindi huo.

"Waziri Mkuu, kiongozi wa dunia. Walijaribu kumuangusha lakini walishindwa," alisema mfuasi huyo.

Profesa wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Jerusalem, Reuven Hazan, anasema ushindi huo wa Netanyahu hautokuwa na athari yoyote katika uchaguzi mkuu ujao. Hazan anasema ushindi huu unamaanisha kwamba amefanikiwa tu kudhibiti uongozi wa chama chake.

Kwa kumshinda kwa urahisi Saar, Netanyahu ameyaweka hai matumaini yake ya kujikinga kutoshitakiwa baada ya kudaiwa kuhusika katika msururu wa madai ya ufisadi mwezi uliopita. 

Netanyahu anataka sana kusalia afisini ili asishitakiwe kwa ufisadi

Netanyahu ambaye ana umri wa miaka sabini anakanusha madai hayo na anawashutumu polisi, viongozi wa mashtaka na na vyombo vya habari kwa kumuendea kinyume.

Benjamin Netanjahu Ministerpräsident von Israel
Waziri Mkuu Benjamin NetanyahuPicha: dpa

Waziri mkuu huyo anataka sana kusalia afisini kwa kuwa hapo ndipo alipo katika nafasi nzuri ya kupambana na madai ya ufisadi yanayomkabili. Sheria ya Israel inawataka maafisa wa umma kujiuzulu iwapo watashtakiwa kwa uhalifu ingawa sheria hiyo haimgusi waziri mkuu aliye madarakani.

Netanyahu anatazamiwa kuitumia nafasi hiyo kama jukwaa la kuwakosoa waendesha mashtaka. Anaweza pia kujenga ushawishi wa kisiasa kwa wabunge wengi kwa matumaini ya kuungwa mkono katika azma yake ya kutofunguliwa mashtaka kwa madai hayo yanayomkabili.