1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Ulaya kutuma majeshi Afrika ya Kati

Admin.WagnerD18 Desemba 2013

Ufaransa imesema kwamba nchi nyingine za Ulaya zitatuma wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusaidia vikosi vya Ufaransa na vya nchi za Kiafrika katika juhudi za kuyanyang'anya silaha makundi yanayohasimiana.

https://p.dw.com/p/1Abqk
Ufaransa ndiyo nchi pekee ya Ulaya iliyo na wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
Ufaransa ndiyo nchi pekee ya Ulaya iliyo na wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: picture-alliance/AP

Kuwepo kwa mpango huo wa nchi nyingine za Ulaya kupeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kumetangazwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius, ambaye hata hivyo hakutaja majina ya nchi hizo. Awali waziri huyo alikwishasema kuwa Poland, Uingereza, Ujerumani, Uhispania na Ubelgiji ziko tayari kutuma vikosi vyao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mjini Brussels, duru za kijeshi kutoka afisa ambaye hakutaka jina lake litajwe, zilieleza kuwa Ubelgiji ilikuwa tayari kutuma wanajeshi 150 ambao watakuwa na jukumu la kudhibiti usalama katika uwanja wa ndege mjini Bangui.

Wakati huo huo serikali ya Uhispania imeridhia mpango wa kutuma ndege aina ya Hercules ya kusafirisha vifaa vya kijeshi, ambayo itakuwa na vifaa vya ukarabati vitakavyosindikizwa na wanajeshi 60. Hata hivyo nchi hiyo inahitaji kibali cha bunge kabla ya kutekeleza uamuzi huo.

Maelfu ya wakazi wa mji mkuu Bangui wameyahama makazi yao kutokana na ghasia
Maelfu ya wakazi wa mji mkuu Bangui wameyahama makazi yao kutokana na ghasiaPicha: Fred Dufour/AFP/Getty Images

Wanajeshi 850 wawasili Bangui

Haijawa bayana kama nchi hizo zitaisaidia Ufaransa katika operesheni kwenye uwanja wa mapigano. Marekani tayari imeanza kutoa msaada wake kwa kuwasafirisha wanajeshi wa Burundi wapatao 850 hadi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakiwa sehemu ya kikosi cha wanajeshi 6000 wa kiafrika wanaotarajia kuunda ujumbe wa Umoja wa Afrika utakaojulikana kama MISCA. Marekani pia imeahidi kutoa msaada wa dola milioni 100 kuusaidia ujumbe huo.

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Linda Thomas Greenfield amesema nchi yake inahangaishwa na kuongezeka kwa ghasia zenye misingi ya kikabila katika maeneo mengi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Thomas Greenfield ameliarifu bunge la nchi yake kuwa anapanga safari kuelekea katika nchi hiyo, akisindikizwa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko baada ya mapinduzi ya mwezi Machi, ambayo yaliwaweka madarakani waasi waliokuwa chini ya muungano uitwao Seleka, ulioongozwa na Michel Djotodia ambaye alitangazwa kuwa rais mpya. Hata hivyo, wengi wa waasi hao walikuwa wahuni, na walianzisha vurugu ambazo jeshi la serikali lilishindwa kuzidhibiti.

Doria barabarani

Umoja wa Mataifa umesema kuwa watu wasiopungua 600 wamekwishauawa, na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Jana, wanajeshi wa Ufaransa waliingia katika wilaya Boy-Robe iliyo kaskazini mwa mji mkuu, Bangui, ambayo ni ngome ya wanamgambo wa kikristo ambao wanapigana dhidi ya wengine wa kiislamu.

Wanajeshi wa Ufaransa wamekosolewa kushika doria kwenye barabara kuu wakiepuka vichochoroni yaliko machafuko
Wanajeshi wa Ufaransa wamekosolewa kushika doria kwenye barabara kuu wakiepuka vichochoroni yaliko machafukoPicha: S.Kambou/AFP/GettyImages

Lakini wakazi wa mji huo wamewakosoa wanajeshi hao wa Ufaransa, kwa kushika doria kwenye barabara kubwa, huku wakiacha mitaa ya mabanda ambako uporaji na machafuko yenye misingi ya kidini yamekuwa yakiendelea.

Tangu kuibuka kwa mzozo mwaka mmoja uliopita, watu zaidi ya laki saba nchini kote Jahmuri ya Afrika ya Kati wameyahama makazi yao, na wapatao 75,000 wamevuka mpaka na kukimbilia nje ya nchi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman