1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi kadhaa zachukua tahadhari ya janga la virusi vya Corona

Sekione Kitojo
27 Februari 2020

Serikali za mataifa kadhaa zinachukua hatua kupambana na janga linaloelekea kuikabili dunia la virusi vya Corona wakati idadi ya watu  walioambukizwa nje ya China ikipita wale walioambukizwa ndani ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3YVMf
Iran Corona-Kranke im Krankenhaus
Picha: Yjc

Australia  imeanzisha  hatua  za  dharura na  taiwan  imepandisha kiwango  cha  kuchukua  hatua  kuhusu  janga  hilo kwa  kiwango cha juu, siku moja  baada  ya  rais  wa  Marekani Donald Trump  kumteua makamu  wake  wa  rais  Mike Pence, katika  nafasi  ambayo atahusika  na  mapambano  dhidi  ya  mzozo  huo  wa  kiafya unaoikabili  dunia.

Russland Moskau | Coronavirus | Chinesischer Passagier, Kontrolle Temperatur
Upimaji wa watu kuhusu virusi vya coronaPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Golovkin

Marekani  na  Korea  kusini  zimeahirisha  luteka  yao ya  pamoja  ya kijeshi  ili  kupunguza  kusambaa  kwa  virusi  hivyo, ambavyo vimejitokeza  katika  maeneo  ya  mbali  na  China, sehemu  virusi hivyo  vilipoanzia , katika soko linalouza nyama  za  wanyama  pori katika  mji  wa  Wuhan.

Waziri  mkuu  wa  Australia  Scott Morrison  amesema  nchi  yake , ambayo  ina watu 23  walioambukizwa  virusi hivyo, inachukua  hali hiyo  katika  kiwango  cha  janga  na  mahospitali  yamepewa  amri kuhakikisha  madawa  ya  kutosha  yanapatikana, pamoja  na  vifaa vya  kuwakinga  wauguzi  na wafanyakazi.

Masoko  ya  hisa  yameporomoka  zaidi, bei  ya  mafuta  pamoja  na hati fungani  za  serikali  ya  Marekani zikiingia  katika  hali ya mdororo wakati  ishara  zaidi  za  kusambaa  kwa virusi  hivyo duniani  zikiongeza  hofu  ya  kutokea janga  la  mzozo  huo.

Watu  zaidi  ya  80,000  wameambukizwa  virusi  vya  corona , na watu 2,800  wamefariki, wengi  wao  nchini  China.  Korea kusini imeripoti watu  171 walioambukizwa, na  kufikisha  watu 1,766 kwa jumla  walioambukizwa.  China imeripoti watu wapya 433 walioambukizwa na  watu wengine 29 wamefariki.

Spanien Kanarische Inseln | Hotelangestellter trägt Gesichtsmaske als Schutzmaßnahme: Hotel wegen Coronavirusfall abgeriegelt
Shughuli za safari na utalii pia zimeathirika katika nchi mbali mbali zilizo na maambukizi ya virusi vya coronaPicha: Reuters/C. Betts

Iran haitaiweka miji katika karantini

Rais  wa  Iran  Hassan Rouhani  amesema  jana  kuwa  nchi  hiyo haina  mipango  ya  kuweka miji  yake  katika  karantini  kutokana  na maambukizi na  vifo  nchini  humo  kutokana  na  virusi  vya  corona, ambapo  wizara  ya  afya  imesema  watu 19 wamefariki nchini humo.

Saudi Arabia imesitisha  leo  utoaji  wa  visa  kwa  watu  wanaofanya ziara  katika  maeneo  matakatifu  kwa ajili  ya  ibada ya  hija  ndogo ya  Umrah,  hatua  ambayo  imesababishwa  na  hofu  ya  virusi  vya Corona  na  pia kuna wasi wasi kuhusu  ibada  ya  kila  mwaka  ya hija.

Washington Rede Mike Pence Beziehungen USA China
Makamu wa rais wa Marekani Mike PencePicha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Nchi  hiyo  ya  kifalme , ambayo  inakuwa  mwenyeji  wa  mamilioni ya  mahujaji  kila  mwaka  katika  miji  ya  Mecca  na  Medina , pia imesitisha  visa  kwa  watalii  kutoka  katika  nchi  ambazo zimeripotiwa  kuwa  na  maambukizi  wakati  hofu  ya  kutokea  janga la  virusi  hivyo  ikiongezeka.

Shirika  la  taifa  la  utalii  nchini Urusi  leo  limelitaka  shirika  la  taifa la  safari za  kitalii  kusitisha  safari  hizo  zote kwenda  Italia, Korea kusini  na  Iran  hadi  pale suala  hilo  la  virusi  vya  corona litakapodhibitiwa  katika  nchi  hizo.