1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi kadhaa hazijatia saini mkataba wa mwaka 1990 wa umoja wa mataifa

5 Aprili 2006

Nchi 10 zilizo wenyeji wa kundi kubwa la wahamiaji wa kimataifa hazijatia saini wala kuthibitisha mkataba wa umoja wa mataifa wa mwaka 1990 wenye lengo la kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/CHnV

Ni wazi kabisa kuwa nchi hizi hazitaki kuchukuwa jukumu la kulinda maslahi ya wahamiaji walio katika nchi hizo…hayo yamesemwa na afisa mmoja mkuu wa umoja wa mataifa ambae hakutaka kujulikana.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya umoja wa mataifa ya mwaka 2005 zaidi ya wahamiaji milioni 102 wapo katika nchi kumi zikiwemo Marekani, Urusi, Ujerumani, Ukraine, Ufaransa, Saudi Arabia, Canada, India, Uingereza na Uhispania.

Kufikia mwaka jana Marekani iliongoza kwa kuwa na wahamiaji milioni 38.4 ikifuatiwa na Urusi ambayo ilikuwa na jumla ya wahamiaji milioni 12.1 Ujerumani wahamijai milioni 10.1 Ukraine wahamiaji milioni 6.8 na Ufaransa wahamiaji milioni 6.5.

Idadi ya wahamiaji wa kimataifa iliongezeka ulimwenguni kote kutoka watu milioni 175 hadi watu milioni 191 kati ya mwaka 2000 na 2005.

Sita kati ya watu 10 au takriban wahamiaji milioni 115 wanaishi katika nchi tajiri duniani lakini wanaendelea kunyimwa haki zao za kimsingi, kwengineko saba kati ya wahamiaji 100 ni wakimbizi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya umoja wa mataifa, nusu ya idadi ya wahamiaji ni wanawake, robo tatu ya wahamiaji hawa wa kimataifa wanatoka katika nchi 28 na wengi wao wanaishi nchini Marekani.

Ripoti hii ya umoja wa mataifa inaendelea kufafanua juu ya mkataba wa mwaka 1990 juu ya wafanyakazi wahamiaji na haki za kimsingi na uhuru wanaostahili kuwa nao pamoja na familia zao.

Mkataba huo wenye lengo la kulinda haki za wahamiaji ulipitishwa na umoja wa mataifa tangu Desemba mwaka 1990 na kuanza kutumika mwezi Julai mwaka 2003, lakini cha kushangaza ni kwamba hadi kufikia mwezi uliopita bado mkataba huo ulikuwa bado haujatiwa saini na nchi kadhaa.

Kati ya nchi wanachama 191 ni nchi 34 pekee ndio tayari zimeshatia saini mkataba huo na nchi hizo sizo miongoni mwa nchi zinazo wakarimu wahamiaji kwa wingi imesema ripoti hiyo inayojulikana kama Uhamiaji na Maendeleo ya Kimataifa.

Kwa sasa maswala haya yanajadiliwa katika mkutano wa kijamii,kiuchumi na uhamiaji wa kimataifa unaohudhuriwa na kamisheni ya umoja wa mataifa juu ya idadi ya watu na maendeleo unaofanyika mjini New York.

Bibi Thoraya Ahmed Obaid mkurugenzi wa tume ya idadi ya watu ya umnoja wa mataifa amesema kwamba maswala kama vile kuendelea kutokomea watalaamu wa afya kutoka nchi maskini kuelekea katika nchi tajiri yanapaswa kuzingatiwa na jamii ya kimataifa.

Nchi nyingi hususan bara la Afrika linapoteza kila kukicha madaktari, wauguzi wasaidizi na wafanykazi wengine katika sekta ya afya hali ambayo inazidisha matatito hasa katika nchi zinazo kumbwa na idadi kubwa ya watu wanougua maradhi ya UKIMWI.

Hivyo basi bibi Thorara ameyahimiza mataifa kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za kibinadamu katikasera za uhamiaji na kushirikiana katika vita dhidi ya biashara ya wahamiaji haramu ulimwenguni ikiwa ni pamoja na bishara haramu ya kuwauza watu na kuwasafirisha kinyume cha sheria.