1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO haitosita kuchukua hatua dhidi ya Urusi

Amina Abubakar Sekione Kitojo
27 Juni 2019

Jumuiya ya kujihami ya Nato imesema itajibu kwa njia tofauti iwapo Urusi itashindwa kuheshimu makubaliano ambayo muda wake wa mwisho wa kuyatekeleza ni Agosti 2, ya kudhibiti uundaji wa makombora ya masafa ya kati.

https://p.dw.com/p/3LAaa
Albanien, Tirana: Pressekonferenz mit Premierminister Rama und Jens Stoltenberg
Picha: DW/A. Ruci

Akizungumza katika mkutano na Mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya kujihami NATO mjini Brussels, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Jens Stoltenberg  amesema  mawaziri hao tayari wamekubaliana kuchukua hatua hizo iwapo Urusi haitakubali kurejea katika utekelezaji wa makubaliano ya kudhibiti uundaji wa makombora ya masafa ya kati.

Jens Stoltenberg ameyazungumza hayo  katika mkutano wa siku mbili ulianza leo kujadili suala hilo mjini Brussels. Jens amesema hatua itakayochukuliwa itafikiriwa na itakuwa hatua ya kujilinda.

Russland Vizeaussenminster Sergei Ryabkov
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei RyabkovPicha: picture-alliance/dpa/Sutnik/V. Belousov

Marekani inaishutumu Urusi kukiuka makubaliano ya kudhibiti uundwaji wa makombora ya masafa ya kati INF yaliotiwa saini na pande zote mbili mwaka 1987, yanayokataza utengenezwaji wa makombora ya ardhini yanayoweza kubeba silaha za nyuklia  na kuwa na uwezo wa kurushwa umbali wa kilomita 500 hadi 5,500.

Marekani imesema itajiondoa katika mpango huo iwapo Urusi haitoheshimu makubaliano hayo ifikapo Agosti 2. Hata hivyo Urusi yenyewe inakana madai ya Marekani na tuhuma za NATO kwamba imekiuka mpango huo, kwa kutengeneza mfumo wa makombora aina ya  9M729 yanayojulikana na Jumuiya ya NATO kama SSC-8.

Ujerumani yasema Urusi bado ina nafasi ya kuheshimu makubaliano

Urusi kupitia naibu waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Ryabkov imesema inafuatilia kwa karibu muenendo wa NATO na iko tayari kwa lolote.  Huku ikitishia pia kujiondoa katika makubaliano hayo.

Stoltenberg amesema jumuiya hiyo  haina nia ya kutangaza kambi mpya ya makombora ya Nyuklia barani ulaya huku akisisitiza kuwa jukumu lao ni kuhakikisha inadhibiti kikamilifu makombora hatari.

USA UN-Sicherheitsrat Ursula von der Leyen
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Katibu Mkuu huyo wa Nato amesema Urusi bado ina nafasi ya kutekeleza makubaliano ya INFna kwamba maelezo zaidi yatatolewa katika mkutano wao wiki ijayo na mabalozi wa Jumuiya ya NATO pamoja na Urusi.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula Von der Leyen amesema kitu muhimu kilichobakia ni kuwa na muungano wa kweli na NATO akimaanisha kuwa itakuwa vyema iwapo Urusi itarejea na kuheshimu makubaliano hayo.

Vyanzo :dpa/Reuters