1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kujadili mzozo wa Urusi na Ukraine

4 Desemba 2018

Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka nchi 29 wanachama wa jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO wanakutana mjini Brussels kujadili miongoni mwa mengine kisa cha Urusi kuzikamata meli na mabaharia 24 wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/39PhR
Treffen der NATO-Verteidigungsminister in Brüssel
Picha: DW/I. Sheiko

Wakati wa mkutano huo wa siku mbili mawaziri hao watakutana na mwenzao wa Ukraine Pavlo Klimkin  ambaye anajaribu kusaka uungwaji mkono wa kimataifa kwa nchi yake kuhusiana na kisa cha makabiliano na Urusi kwenye bahari ya Azov.

Viongozi wa NATO wanatarajiwa kutangaza uuangaji mkono kwa Ukraine lakini hawatatoa ulinzi kwa meli zinazoingia kwenye bandari za Ukraine au msaada wowote ziada wa kijeshi mbali ya ule unaotolewa hivi sasa.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema jumuiya hiyo inafuatilia kwa karibu kinachoendelea katika bahari nyeusi na kutoa wito wa kuwepo utulivu na kuitaka Urusi kuziachia meli na mahabaria wa Ukraine wanaoshikiliwa.

Novemba 25 Urusi ilizikamata meli tatu za jeshi la majini la Ukraine katika rasi ya Crimea, eneo ambalo Urusi ililipoka kutoka Ukraine mwaka 2014.

Kisa hicho kiliibua wasiwasi wa kuzuka mzozo wa kijeshi baina ya nchi hizo jirani.

Wasiwasi unapungua?

Brüssel Jens Stoltenberg, NATO-Generalsekretär
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/D. Aydemir

Wakati huo Ukraine imeripoti leo kuwa Urusi imezifungua kwa sehemu, bandari za Ukraine katika bahari ya Azov siku moja baada ya katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kuitaka Urusi kumaliza makabiliano ya majini na Ukraine kwenye eneo hilo la bahari. 

Waziri wa miundombinu wa Ukraine Volodymyr Omelyan amesema bandari za Berdyansk na Mariupol zimefunguliwa kwa sehemu na meli zimeanza kuruhusiwa kuingia na kutoka kwenye bandari za Ukraine kupitia mlango bahari wa Kerch.

Viongozi wa Ulaya waliutumia mkutano wa G20 mwishoni mwa juma nchini Argentina kumshinikiza rais wa Urusi Vladimir Putin kumaliza uhasama uliozuka na Ukraine lakini haitarajiwi kuwa nchi za magharibi zitachukua hatua ziada dhidi ya Urusi wakihofia kuukoleza mzozo huo.

Ikulu ya Urusi, Kremlin ilitangaza jana kuyakataa mapendekezo ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ya kutaka kuanzishwa tena mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin amesema muundo wa mazungumzo ya hapo kabla ambayo Ujerumani na Ufaransa zilikuwa wapatanishi hayahusiani na makabiliano ya karibuni kati ya walinzi wa pwani wa Urusi na jeshi la majini la Ukraine karibu na eneo linalozozaniwa la Crimea.

Kansela Merkel alisema kupitia msemaji wake kuwa  alikubaliana na rais Putin kuanzisha mazungmzo  juu ya mgogoro huo mpya katika muundo unaojulikana kama "Normandy” lakini Urusi imesema muundo huo ulihusu mazungumzo ya kuheshimiwa makubaliano ya Minsk ya kusitisha mapigano katika mikoa ya magharibi ya Ukraine na si vinginevyo.

Ukraine yafanya upekuzi makanisani

Hayo yanakuja wakati siku ya jumatatu mamlaka nchini Ukraine ziliyavamia na kuyafanyia upekuzi makanisa matatu ya Orthodox yenye mafungamano na Urusi kwa madai ya ukiukaji wa sheria ya usawa wa kuabudu na kuamini dini.

Ukraine | St. Andreaskirche in Kiew
Picha: picture-alliance/dpa/ ITAR-TASS/V. Sindeyev

Maafisa wa polisi walifanya pia upekuzi kwenye makazi ya makasisi wa makanisa hayo ambao walitangaza utii kwa tawi la kanisa la Orthodox la Urusi lakini msemaji wa polisi wa mkoa wa Kaskazini wa Ukraine amesema hakuna aliyekamatwa. .

Kanisa la Orthodox la Ukraine lilipata ushindi wa kuwa huru na kujitenga kutoka Urusi katika maamuzi yaliyoshangiliwa nchini huko lakini yamezusha hasira nchini Urusi.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Iddi Ssessanga