1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Narendra Modi aahidi kuipatika Uganda mashine ya saratani

Swaibu Ibrahim24 Julai 2018

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amefanya ziara nchini Uganda na kuahidi kuipatia nchi hiyo mashine ya kisasa ya kutibu ugonjwa wa saratani. Modi anaelekea Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS.

https://p.dw.com/p/321ai
Ruanda Ankunft des indischen Ministerpräsidenten Narendra Modi in das "India-Rwanda business forum"
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Nchini Uganda, Modi anatarajiwa kukutana na jamii ya Wahindi na kulihutubia bunge la nchi hiyo siku ya Jumatano. Pia atashiriki mkutano wa kilele wa wafanyabiashara wa Uganda na India, kabla ya kuelekea nchini Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS.

Mara baada ya kuwasili mjini Entebbe, Modi alikutana na mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni ambapo wawili hao walifanya mazungumzo na kusaini mikataba kadhaa ya kibishara kama alivyofafanua rais Yoweri Museveni.

Yoweri Museveni Präsident Uganda
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: Imago/ITAR-TASS/A. Shcherba

"Kwa upande watu tumesisitiza juu ya biashara, uwekezaji na utalii, kwa sababu haya nndiyo mambo matatu yanayoweza kuwaweka watu pamoja, ambako tunafanya kazi kwa ajili ya manufaa yetu sote. Tunapoweza kusaidia maendelea ya watu wa India kwa kununua bidhaa zao, na wanaweza kusaidia maendeleo yetu kwa kununua bidhaa zetu."

Ukosefu wa urari wa kibiashara

Awali Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya nje Patrick Mugoya alisema viongozi hao wangejadili usawa wa kibishara baina ya mataifa yao. Kulingana na takwimu za benki kuu ya Uganda, nchi hiyo iliagiza bidhaa za thamani ya dola milioni 774 kutoka India, huku nchi hiyo ikiiuzia India bidhaa zenye thamani ya dola milioni 38 tu.

Waziri Mkuu Modi amema nchi yake itaipatia Uganda mashine mpya ya kutibu ugonjwa wa saratani.

"Kama ishara ya urafiki wetu kwa watu wa Uganda, serikali ya India imeamua kutao mashine ya kisasa ya matibabu ya saratani kwa taasisi ya saratani ya Kampala. Nina furaha kubainisha kwamba mashine hii siyo tu itatimiza mahitaji ya marafiki zetu wa Uganda, lakini pia mahitaji ya marafiki zetu kutoka mataifa ya Afrika Mashariki."

Flash-Galerie Alzheimer Diagnostik
Waziri mkuu Modi ameahidi kuipatia Uganda mashine ya kisasa ya saratani.Picha: CHROMORANGE

Uganda ina jamii kubwa ya  Wahindi, likiwemo kundi la wamiliki wa viwanda waliofanikiwa baada ya kurudi kudai mali zao walizopokonywa wakati wa utawala wa Rais Idi Amin. Mwaka 1972, Amin aliamuru kufukuzwa kwa watu wa jamii ya Asia, wengi wao wakiwa Wahindi, kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki, akisema alitakwa kuurejesha uchumi mikononi mwa wenyeji.

Wahindi wataka kutambuliwa kama kabila

Sehemu kubwa ya mali walizonyanganywa zimerejeshwa kwa wamiliki wake wa awali chini ya utawala wa Rais Museveni. Wafanyabiashara wenye asili ya India wamewekeza pakubwa katika sekta uzalishaji, usindikaji w abidhaa za kilimo na dawa nchini Uganda.

Na sasa jamii hiyo inataka kutambuliwa kikatiba kama mmoja ya makabila ya Uganda, jambo ambalo nchi jirani ya kenya ilifanikisha mwaka uliopita. Mwaka 2015 aliwaalika viongozi wa Kiafrika mjini New Delhi kwa ajili ya mkutano wa kilele wa India na Afrika ambao ndiyo ulikuwa mkubwa zaidi wa aina yake.

Mwandishi: Swaibu Ibrahim

Mhariri: Mohammed Khelef