1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda achakuliwa kuwa kiongozi katika chama cha waasi wa Kihutu.

30 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CEyo

Mfanyakazi wa zamani wa umoja wa mataifa anayetuhumiwa kushiriki katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 ambaye hivi sasa ni mkimbizi nchini Ufaransa amechaguliwa katika nafasi ya juu katika chama cha waasi wa Kihutu.

Chama hicho cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda FDLR, kimesema jana kuwa Callixte Mbarushimana amechaguliwa kuwa makamu katibu mkuu wa chama hicho katika mkutano uliofanyika mjini Bonn siku ya Jumamosi.

Mbarushimana anatuhumiwa kwa kuhusika katika mauaji ya watu 33, ambao wameuwawa wakati wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda na Wahutu wenye msimamo mkali dhidi ya Watutsi ambao ni wachache nchini humo pamoja na Wahutu wenye msimamo wa wastani na kusababisha watu 800,000 kuuwawa.

Wakati huo huo mahakama moja nchini Ubelgiji imewahukumu wafanyabiashara wawili wa Rwanda kwenda jela kwa miaka 12 kila mmoja kwa uhalifu wa kivita katika mauaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda. Mahakama hiyo imempata Etienne Nzabonimana na mdogo wake Samuel Ndashyikirwa na hatia ya kuongoza mauaji hayo katika jimbo la Kibongo.