1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Venezuela na ziara ya Papa Francis Magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Februari 2019

Mada mbili tu zimehodhi magazeti ya Ujerumani hii leo: Kinyang'anyiro cha kuania madaraka nchini Venezuela na ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis katika nchi mojawapo ya bara Arabu.

https://p.dw.com/p/3Cj5w
VAE Papst Franziskus in Abu Dhabi
Picha: Reuters/A. Jadallah

Tunaanzia Amerika Kusini, nchini Venezuela ambako muda aliopewa rais Nicolas Maduro na jumuia ya kimataifa wa kuitisha uchaguzi mkuu umeshamalizika. Nchi nyingi zimeamua kumtambua spika wa bunge Juan Guaidos kuwa rais wa mpito. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linakosoa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya kuelekea suala la Venezuela na kuandika: "Walipompa muda, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya waliamini mwisho wa enzi za Maduro unakaribia. Walitaraji wamarekani wangefanikiwa kuwashawishi majenerali wamuunge mkono Guaido. Kujiingiza nchi za Ulaya katika mzozo wa Venezuela sio chochote chengine isipokuwa kushika mkia. Na sasa nchi za Ulaya zinajionea matokeo yake. Umoja wa ulaya bado hauzungumzi kwa sauti moja katika siasa yake ya nje."

Italia yazuwia mpango wa Umoja wa ulaya kumtambua Guaido

 Gazeti la Badische Zeitung nalo pia linakosoa msimamo wa Umoja wa Ulaya na kuandika: "Wenye kuweka muda wanabidi angalao wawe na msimamo mmoja. Muda sasa umeshamalizika bila ya Maduro kutekeleza masharti yaliyowekwa-Na zaidi ya hayo hayakufika hata nusu mataifa ya Ulaya yaliyotangaza jumatatu iliyopita kumtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido kuwa rais halali. Ni aibu kweli kweli hiyo kwa Umoja wa Ulaya. Wameshindwa kwasababu ya msimamo wa italia na utaratibu wa maamuzi kupitishwa kwa sauti moja. Kwa sasa hakuna ajuaye kama walioshinda ni wale waliojizuwia au wengine mfano wa Ujerumani wanaomuwekea matumaini  Guaido katika mzozo huu wa Venezuela. Hatari iko pande zote mbili. Ingawa kuzidi kumshinikiza Maduro ni sawa, kwasababu bila ya hivyo hakuna ufumbuzi unaoweze kupatikana mjini Caracas, lakini hatari itakuwa kubwa zaidi pale mzozo wa kuania madaraka utakapogeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Venezuela.

Papa Francis ahimiza masikilizano kati ya waumini

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka bara Arab inakomalizika ziara ya kihistoria ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Papa Francis huko Abu Dhabi. Gazeti la "Westfalenpost" linamulika umuhimu wa ziara hiyo na kuandika: "Kwa kufanya ziara hiyo Papa Francis amedhamiria kufungua ukurasa mpya katika uhusiano kati ya waislam na wakristo. Ni dhamir adhimu na muhimu kuliko wakati wowote mwengine. Matatizo yanayoukaba ulimwengu ni mengi  hata bila ya kujumuisha itikadi kali za kidini. Nasaha ya Papa Francis imelengwa pande zote. Kwasababu nchi za magharibi zinaonyesha kuamini  dhana hivi sasa kwamba wakimbizi wa kiislam na wahamiaji ndio chanzo cha matatizo yote yaliyoko na shada hapo inawekwa katika Uislam.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse

Mhariri: Mohammed Khelef