1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kisiasa nchini Congo wazidi kuibua wasiwasi

3 Desemba 2020

Umoja wa Mataifa umetoa onyo kuhusu mzozo wa kisiasa unaoibuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati mvutano wa muda mrefu kati ya Rais Felix Tshisekedi na wafuasi wa Joseph Kabila unaendelea.

https://p.dw.com/p/3mAVs
Bildkombo I Félix Tshisekedi und  Joseph Kabila
Rais Félix Tshisekedi na Joseph Kabila

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ripoti yake kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema ana wasiwasi kuhusu mzozo wa kisiasa ndani ya muungano tawala nchini Congo.

Guterres ameonya kuwa mzozo uliopo unaweza kudhoofisha utulivu wa kisiasa uliopo na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana tangu uchaguzi wa 2018 na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani. Mzozo huo pia unaweza kuathiri juhudi za kushughulikia changamoto za usalama Mashariki mwa nchi hiyo. soma zaidi Mvutano wazidi kuitishia serikali ya Tshisekedi

Ripoti hiyo iliyoonyeshwa Shirika la Habari la AFP, ilifanana na video inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wa Rais wa Congo Meja Jenerali Christian Tshiwewe, alionekana akiwaamuru wanajeshi wake "wasipange njama dhidi ya serikali."

Major Tshiwewe alisema "Ninawahimiza musipange njama dhidi ya serikali kwa kushiriki katika mikutano ya siri, Kuweni wazalendo, muliojaa uaminifu na utiifu kwa mkuu wa nchi."

Demokratische Republik Kongo Félix Tshisekedi
Picha: Giscard Kusema/Press Office President DRC

Vikosi vya jeshi

Vikosi vya jeshi katika ngazi za juu vinatawaliwa na maafisa walioteuliwa na Kabila wakati wa utawala wake, ambaye alijiuzulu mnamo Januari 2019 baada ya miaka 18 kutawala mojawapo ya nchi tete kabisa barani Afrika.

Kujiuzulu kwa Kabila kulionyesha mabadiliko ya kwanza ya amani katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu kupata uhuru kutoka Ubelgiji mnamo 1960. Soma zaidiUpinzani DRC wamuonya Rais Tshisekedi

Rais Tshisekedi katika mchakato wake wa kuleta mageuzi nchini Congo, anakabiliwa na changamoto wakati ambapo analazimika kufanya  kazi ndani ya vizuizi vya muungano unaodhibitiwa na vibaraka wa Kabila.

Mvutano uliibuka wazi baada ya rais Tshisekedi mnamo Julai kuwataja majaji watatu wapya katika Korti kuu, Hatua ambayo Baraza la Katiba, lilipuuzilia mbali malalamiko makali kutoka kwa FCC. Viongozi wa FCC walisusia sherehe za kuapishwa kwa majaji hao mnamo Oktoba 21.

Demokratische Republik Kongo Parlament in Kinshasa
Bunge la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya CongoPicha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Siku mbili baadaye, Tshisekedi alikiri kuwa kumekuwa na kutokubaliana juu ya maswala ya  usalama wa taifa, usimamizi wa mali za serikali, Uhuru wa mahakama pamoja na mipango na taratibu za uchaguzi.

Kulingana na Msemaji wa rais, mnamo Novemba 2, rais Tshisekedi alizindua mazungumzo na "vikosi vya kisiasa na kijamii, kwa lengo la kuwaunganisha kwa kile alichokitaja kama kuwa karibu na maono ya pamoja ya utawala unaojulikana kama "umoja mtakatifu wa taifa."

Maamuzi ya mashauriano

Rais Tshisekedi sasa anajiandaa kutangaza maamuzi yake baada ya mashauriano hayo. Hata hivyo siku atakayotoa tangazo hilo bado ni kitendawili hasa swala la ni kipi atakachokisema limeibua uvumi mkubwa katika mji mkuu Kinshasa.

Viongozi wa chama cha rais, UDPS, wamekuwa wakimtaka Tshisekedi aachane na mkataba ambao haukuchapishwa ambao aliunda na Kabila mnamo Januari 2019.

Wabunge wanaomuunga mkono Kabila wanachukua viti 305 kati ya 500 katika Bunge la Kitaifa, ambalo uchaguzi ulifanyika mnamo Desemba 2018 pamoja na kura ya urais. Soma Zaidi Mpasuko mkubwa muungano wa Tshisekedi, Kabila Congo

Katika Bunge la Seneti, FCC ina zaidi ya viti 90 kati ya viti 109, ambayo nafasi moja ilipewa Kabila mwenyewe, aliyetajwa kuwa seneta wa maisha. FCC pia inashikilia karibu majimbo yote 26 ya mkoa.

 

AFP/