Mzozo wa Bahari ya China Kusini watishia biashara kimataifa
20 Agosti 2024Enzi ya baada ya mripuko wa virusi vya UVIKO-19 imekuwa ngumu kwa biashara ya kimataifa. Kufungwa kwa viwanda na vizuizi vya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo kulisababisha kucheleweshwa kwa usambazaji wa bidhaa kote duniani na pia kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei za bidhaa. Mnamo mwaka 2021, Mfereji wa Suez ulifungwa kwa wiki moja baada ya meli ya kubeba mizigo kukwama.
Mashambulizi dhidi ya meli yaliyofanywa na waasi wa Kihouthi wa Yemen na Iran katika kipindi cha miezi 10 iliyopita yamelazimisha meli za mizigo kubadilisha njia kutoka Bahari ya Shamu kupitia Afrika. Na sasa, mvutano unaoongezeka kati ya China na majirani zake umeibua wasiwasi wa kiusalama kuhusu njia nyingine muhimu ya kibiashara: Bahari ya China Kusini.
Bahari ya China Kusini ina uhumimu gani?
Ikiunda sehemu ya magharibi mwa Bahari ya Pasifiki, Bahari ya China Kusini iko kati ya kusini mwa China, Taiwan, Ufilipino, Indonesia, Vietnam, Thailand, Cambodia na Malaysia.
Kulingana na Kongamano la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD, takriban thuluthi moja ya biashara ya kimataifa ya baharini hupitia njia hiyo ya bahari ya kilomita milioni 3.5 za mraba kila mwaka.
Takriban 40% ya bidhaa za petroli zinazouzwa ulimwenguni kote husafirishwa kupitia bahari kila mwaka.
Kulingana na Kituo cha Masomo ya Kimkakati na Kimataifa CSIS chenye makao yake mjini Washington Marekani, mnamo mwaka wa 2016, bidhaa zenye thamani ya dola trilioni 3.6 zilisafirishwa kupitia baharini.
Soma pia: Biden aapa kuzilinda Ufilipino na Japan katikati mwa mvutano na China
Data za CSIS pia zinaonyesha kuwa maelfu ya meli za mizigo hupitia Bahari ya China Kusini kila mwaka na kubeba takriban asilimia 40 ya bidhaa za biashara za China, thuluthi moja za India na asilimia 20 za Japan pamoja na mataifa mengine duniani.
Kati ya mataifa yote ya bara Asia, usalama wa kiuchumi wa nchi hizo tatu unafungamana kwa karibu zaidi na uendeshaji mzuri wa biashara katika njia hiyo ya bahari. Bahari ya China Kusini ni njia muhimu kwa biashara ya ndani ya Asia na pia kwa biashara na ulimwengu wote, haswa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika.
Nini kinaifanya Bahari ya China Kusini kuwa suala tata?
China inadai kumili takriban Bahari yote ya China Kusini hatua inayokasirisha nchi jirani zinazosema azma ya kimaeneo ya China inaingilia maeneo yao ya kipekee ya kiuchumi. China ilipuuza uamuzi wa mwaka 2016 wa mahakama ya kimataifa ya usuluhishi huko The Hague, Uholanzi, kwamba Beijing haina msingi wa kisheria au wa kihistoria wa madai yake makubwa chini ya sheria za kimataifa.
Bahari ya China Kusini inakadiriwa kuwa na takriban mita trilioni 5.38 za gesi asilia iliyothibitishwa na inayodhaniwa na akiba ya mafuta ya mapipa bilioni 11 . Haya ni kulingana na Usimamizi wa Habari za Nishati ya Marekani.
Tangu mwishoni mwa mwaka jana, biashara ya kimataifa imeathiriwa na mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran katika Bahari ya Shamu karibu na Yemen.
Waasi hao waliamuru mashambulizi ya droni na makombora dhidi ya meli za kibiashara kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza.
Soma pia: China yaionya Ufilipino juu ya mzozo wa bahari ya China Kusini
Kampuni kubwa za usafirishaji zimeelekeza meli zao kutoka njia ya Bahari ya Shamu inayojumuisha Mfereji wa Suez. Badala yake, meli za mizigo hupitia njia ya Cape of Good Hope kusini mwa Afrika, na kuongeza takriban siku 10 kwa wastani za safari kutoka Asia hadi Ulaya.
Hatua hiyo imeongeza gharama za usafirishaji kutokana na bei ya juu ya bima na dizeli, ambazo zilisababisha ucheleweshaji katika bandari za mizigo barani Ulaya na Asia.
Ikiwa mvutano kati ya China na majirani zake utazidi kuzorota, inaweza kufungua sehemu ya tatu ya mzozo wa safari za meli duniani.
Kampuni za safari za meli zinaweza kuanza kuepuka sehemu za Bahari ya China Kusini.
Kucheleweshwa kwa mizigo pamoja na kupandishwa kwa bei huenda kukasababisha uhaba wa bidhaa na kupunguza mapato muhimu kwa bandari kuu za Asia, zikiwemo zile za Singapore, Malaysia na Taiwan.