1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Umoja wa Mataifa waafiki makubaliano endelevu ya kiutu, Gaza

28 Oktoba 2023

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kwa wingi mkubwa azimio lisilo na uzito wa kisheria linalotaka "makubaliano ya mara moja, ya kudumu na endelevu ya kibinadamu" katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4Y8Xf
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kuruhusu ufikishwaji wa misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kuruhusu ufikishwaji wa misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Bebeto Matthews/AP Photo/picture alliance

Mataifa 120 yalipiga kura ya kuunga mkono azimio hilo lililowasilishwa na mataifa ya Kiarabu. Mataifa 14 yalipinga azimio ilo ikiwa ni pamoja na Israel, Marekani na Australia. Mataifa 45 hayakupiga kura. Wachambuzi wanasema, matokeo haya pamoja na mengine, yameashiria mgawanyiko ndani ya mataifa ya magharibi, na hasa baada ya Ufaransa kupigia kura azimio hilo, huku Ujerumani, Italia na Uingereza yakijizuia.

Mapendekezo ya azimio hilo yaliandaliwa na Jordan, ikiungwa mkono na mataifa 22 ya Kiarabu, na kutoa wito huo wa makubaliano ya haraka ili misaada kuweza kuingia Gaza na kusitishwa kwa mapigano. Rasimu ya kwanza ya azimio ililenga tu katika kusitishwa mapigano.

Soma pia:Miito imekuwa ikongezeka ya kufunguliwa kwa njia salama na zisizo na vizuizi za kupitisha misaada ya kiutu hadi Gaza

Israel imekosoa kwa ghadhabu pendekezo hilo, huku balozi wa taifa hilo kwenye Umoja wa Mataifa Gilad Erdan akiliita kuwa ni "takataka" na kusema Israel itaendelea kujilinda.

Miale ya makombora ya Israel yaliyorushwa kuelekea upande wa kaskazini wa Gaza, Oktoba 28, 2023
Miale ya makombora ya Israel yaliyorushwa kuelekea upande wa kaskazini wa Gaza, Oktoba 28, 2023 Picha: Abed Khaled/AP Photo/picture alliance

Huku hayo yakiripotiwa, vikosi vya Israel vimefanya mashambulizi mengine ya ardhini huko Gaza katika wakati ambapo vikosi vyake vinaendelea kujiimarisha kwa uvamizi, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo ambaye amesema utafanyika hivi karibuni.

Karibu Wapalestina 7,300 wameuawa hadi sasa.

Ndege za kivita za Marekani nazo zimeshambulia baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Syria baada ya shambulizi la awali dhidi ya wanajeshi wa Marekani, lililofanywa na na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, hatua inayoibua wasiwasi zaidi kwenye ukanda huo.

Mjini Washington, ikulu ya White House imesema imeiomba Israel kuielezea kuhusu malengo na mkakati wake katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na "namna vita hivi vitakavyomalizwa."

Msemaji wa White House John Kirby amekiri kuziona ripoti kwamba jeshi la Israel linaimarisha mashambilizi kwenye Ukanda huo wa Gaza, ingawa hakutaka kuzungumzia zaidi juu ya mashambulizi hayo.

Akizungumzia kwa upana mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas, ambalo Marekani, Ujerumani na baadhi ya mataifa wanalitaja kuwa ni la kigaidi, Kirby amesema Marekani inaunga mkono kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu misaada ya kiutu kufika Gaza na watu kuondoka kwenye eneo hilo.

Kundi la Hamas lenyewe kwa upande wake limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya haraka wakati mashambulizi ya Israel yakizidi kuwaelemea. Kundi hilo limeyaomba mataifa ya Kiarabu na Kiislamu pamoja na jamii ya kimataifa kuwajibika katika kuhakikisha wanamaliza lilichokiita ''uhalifu na msururu wa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wao.''

Soma pia:UNRWA: Bidhaa ya mafuta yahitajika haraka Gaza