1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar kwazidi kufukuta

17 Machi 2021

Waandamanaji nchini Myanmar wamekabiliana na vikosi vya usalama hii leo huku umoja watawa wa Kibuddha wakitoa mwito kwa utawala wa kijeshi kusitisha matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.

https://p.dw.com/p/3qlNV
Myanmar gewaltsame Proteste gegen Militärputsch
Picha: REUTERS

Waandamanaji nchini Myanmar wamekabiliana na vikosi vya usalama hii leo huku umoja wa watawa wa Kibuddha wakitoa mwito kwa utawala wa kijeshi kusitisha matumizi ya nguvudhidi ya waandamanaji na kulituhumu kundi hilo la wachache lililojihami kwa silaha kwa kuwatesa na kuwauwa raia wasio na hatia tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita. 

Waandamanaji hao walitumia manati kukabiliana na polisi na wengine aliwatupia mabomu ya kutengeneza kwenye chupa za vilevi, katika tukio ambalo ni la nadra la kupambana dhidi ya vikosi vya usalama vinavyokabiliana vikali na waandamanaji hao wanaoyapinga mapinduzi.

Kuongezeka kwa makabiliano hayo kunafuatia tamko la shirika moja kwamba zaidi ya watu 200 wameuawa tangu Februari Mosi. Takriban watu wawili waliuawa wakati wa maandamano hii leo katika eneo la kaskazinimagharibi mwa Myanmar, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari na machapisho ya kwenye mitandao ya kijamii yaliyoonyesha picha za wahanga.

Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji wa wazi kabisa dhidi ya hatua kali na za ukandamizaji zinazochukuliwa na wanajeshi dhidi ya waandamanaji, kamati ya watawa hao iliyoteuliwa na kiserikali ya Sangha Maha Nayaka pia imesema kwenye muswada wa taarifa yake kwamba inakusudia kusimamisha shughuli zake, kama hatua moja wapo ya kuupinga utawala huo.

Inapanga kuchapisha rasmi taarifa hiyo baada ya kuwasiliana kwa waziri anayeshughulikia masuala ya dini kesho Alhamisi.

Papst Franziskus gibt nach einem Besuch im Irak eine Pressekonferenz an Bord eines päpstlichen Flugzeugs
Papa Francis ametoa ombi kwa jeshi la Myanmar kusitisha machafuko nchini humoPicha: Yara Nardi/AFP

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis hii leo ametoa mwito wa kumalizwa kwa machafuko ya umwagaji damu nchini humo. Papa Francis amerejea picha zilizowaonyesha watawa wa kanisa hilo nchini Myanmar wakiwa wamepiga magoti barabarani mbele ya wanajeshi wa usalama, na kusema hata yeye anapiga magoti kwenye mitaa ya Myanmar na kuomba machafuko hayo kusitishwa.

Amesema "Kwa mara nyingine na kwa huzuni kubwa, ninatamani kuzungumza juu ya hali ya kushangaza huko Myanmar, ambapo watu wengi, haswa vijana, wanapoteza maisha yao ili kuleta matumaini kwenye nchi yao. Mimi pia napiga magoti kwenye mitaa ya Myanmar, nami nasema, Acheni vurugu. Umwagaji damu hausuluhishi chochote, mazungumzo yanaweza kuleta suluhu."

Maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa serikali iliyochaguliwa ya Aung San Suu Kyi kwa muda mrefu yalikuwa ya amani lakini hii leo baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji wa mji mkuu wa Yangon, walitawanyika na baada ya muda walirudi wakiwa na kuweka vizuizi vya mifuko vya michanga. Baadhi yao walirusha mabomu ya kutengeneza kwenye chupa za vilevi na wengine walitumia manati kuwalenga wanajeshi, ingawa haikuwa rahisi kuwafikia.

Mashirika: APE/RTRE/AFPE