Mwezi mmoja tangu tetemeko la ardhi kutikisa Uturuki, Syria
6 Machi 2023Shirika la Afya Duniani, WHO lilisema hilo lilikuwa janga baya zaidi la asili kutokea kwenye kanda hiyo ya Ulaya katika muda wa karne moja.
Mwezi mmoja tangu kutokea janga hilo, Uturuki ingali inakumbwa na kibarua kigumu cha kuijenga upya miji iliyoharibiwa, huku maelfu ya watu wakihofiwa wangali wamefunikwa kwenye vifusi. Aidha walionusurika wanaishi kwenye mahema. Uturuki imeahidi ujenzi mpya wa haraka baada ya tetemeko la ardhi.
Hapo jana waokozi waliwaokoa manusura sita waliokwama kwenye jengo la orofa sita tangu tetemeko hilo la Februari sita, kwenye mji wa Sanliurfa kusini mashariki mwa Uturuki. Hayo ni kulingana na ripoti ya shirika la habari la nchi hiyo Anadolu.
Hadi sasa, idadi ya vifo kutokana na janga hilo nchini Uturuki imeongezeka na kufikia watu 45,968. Waziri wa mambo ya ndani ya Uturuki Suleyman Soylu alisema hayo Jumamosi na kuongeza miongoni mwa waliokufa ni wahamiaji 4,267 wa Syria waliokimbia vita nchini mwao. Nchini Syria, maelfu pia wamekufa.
Tetemeko la kwanza lililokuwa na ukubwa wa 7.7 kwenye vipimo vya ritcha, lilifuatwa na jingine la ukubwa wa 7.6 kwenye vipimo vya ritcha. Matetemeko hayo ya ardhi yalitikisa jumla ya mikoa 11 ya kusini mashariki mwa Uturuki, na vilevile kaskazini mwa Syria alfajiri ya Februari sita, wakati watu walikuwa wakilala.
Juhudi za uokozi zingali zinaendelea
Maafisa wa Uturuki wamesema majengo 214,000 yaliporomoka hasa katika mikoa ya Hatay na Kahramanmaras.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi, Syria
Hadi leo, timu za waokozi zingali zinajaribu kuondoa vifusi ambavyo vimetapakaa kote kwenye miji iliyoathiriwa.
Kwa ujumla, takriban watu milioni 14, wameathiriwa na janga hilo, hiyo ikiwa ni moja juu ya sita ya idadi jumla ya watu nchini Uturuki.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema hadi sasa, watu milioni 3.3 wamelazimishwa kuondoka katika maeneo hayo ya matetemeko ya ardhi.
Ukosoaji dhidi ya serikali ya Erdogan kuhusu jinsi ilivyoshughulikia janga hilo
Kumekuwa na ukosoaji mkubwa dhidi ya serikali ya Uturuki kwa namna ambavyo imeshughulikia janga hilo.
Erdogan amedai majira ya baridi kali na theluji kumwagika na kusababisha barabara nyingi kujaa barafu, pamoja na barabara kuharibiwa na matetemeko ya ardhi miongoni mwa masuala mengine, vyote vilichangia udhaifu huo.
UN:Watoto milioni 7 wameathirika kote Uturuki na Syria
Katika mikoa mingine, ukiwemo wa Adiyaman, ghadhabu za waathiriwa ingali tele. Manusura wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wameachwa peke yao wakitumia mikono yao kuwaokoa jamaa zao waliofunikwa chini ya vifusi, kwa sababu hakuna timu za waokozi, wanajeshi au polisi waliowasili kuwasaidia.
Wengine wameelezea hali ya kusikitisha ambapo walishuhudia jamaa zao wakifa machoni pao kwa sababu walikosa nyenzo na vifaa vya kuwavuta kutoka kwenye vifusi.
Erdogan alikiri kuna mapungufu na akaomba msamaha baada ya serikali yake kukosolewa. Alipozuru maeneo ya mkasa alisema si rahisi kuwa tayari haraka iwezekanavyo kukabili janga kubwa kama hilo.
Vyombo vya habari vya upinzani pamoja na wanasiasa , wameulaumu mwendo wa kinyonga wa serikali katika kushughulikia janga hilo.
Wanakandarasi walaumiwa kwa ujenzi duni
Shirika la Hilal Nyekundu pamoja na rais wake Kerem Kinik, wameshutumiwa kwa kuuza vifaa vya misaada kama mahema badala ya kupeana bure kwa waathiriwa.
Tetemeko la ardhi na mwelekeo wa uchaguzi nchini Uturuki
Wanakandarasi pia wamelaumiwa kwa kutofuata kanuni kamili za ujenzi, hali iliyosababisha majengo mengi kuporomoka.
Maafisa wanawashikilia zaidi ya watu 200, wakiwemo wanakandarasi kama sehemu ya uchunguzi.
Miaka kadhaa iliyopita, shirika linaloshughulikia majanga na hali ya dharura la Uturuki lilitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea janga la tetemeko la ardhi. Kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, shirika hilo lilitayarisha mipango ya kufuatwa ili kupunguza hatari za majanga.
Mnamo mwaka 2020, walitabiri kwamba kutatokea tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.5 kwenye vipimo vya ritcha katika mkoa wa Kahramanmaras. Utabiri huo ulitimia Februari 6.
Vyanzo: AFPE, DPAE, DW