1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwendesha baiskeli Froome atimiza ahadi yake

4 Desemba 2015

Chris Froome ametimiza ahadi aliyotoa baada ya kushinda mashindano ya Tour de France, kwa kutoa matokeo ya vipimo alivyofanyiwa kuthibitisha kuwa ni mwanamichezo safi asiyetumia dawa za kuongeza nguvu misuli

https://p.dw.com/p/1HHa6
Tour de France 2015 Chris Froome
Picha: Getty Images/D. Pensinger

Hatua hiyo ilikuwa ya kuwanyamazisha wakosoaji nchini Ufaransa ambao kila mara wameelezea mashaka kama yeye ni mwanamichezo safi asiyetumia dawa za kuongeza misuli nguvu.

Maabara ya mjini London ilipima namna mwili wa Froome unavyotumia hewa ya oxygen, pamoja na nguvu zake na uwezo wa kuyakabili mazingira magumu. Matokeo hayo yamechapishwa kwenye tovuti ya jarida la Esquire.

Froome alinukuliwa na jarida hilo akisema yeye ndiye mwanamichezo pekee anayeweza kusema asilimia 100 kuwa ni msafi kwa sababu hajavunja sheria zozote za mchezo huo, wala kujihusisha na udanganyifu wowote.

Huku kukiwa na mashaka katika mchezo wa uendeshaji baiskeli baada ya Lance Armstrong kupokonywa mataji yake saba ya Tour de France kwa kupatikana na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku, vipimo alivyofanyiwa Froome huenda visiwashawishi kabisa wale wanaomtilia mashaka.

Froome mshindi wa Tour de France 2013 na 2015 hajawahi kugunduliwa kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini lakini lakini baadhi ya watangazaji wa mchezo huo walimkosesha usingizi wakati alipopata ushindi wake mwezi Julai.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo