1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kijana mwenye niqab ashiriki mashindano ya chess ya wanawake

17 Aprili 2023

Kijana aliyevalia nikabu na miwani alicheza raundi nne za mashindano ya wazi ya Chess ya wanawake ya Nairobi kabla ya kufichuliwa. Alisema alisukumwa na hali ngumu ya maisha na uwezekano mdogo wa kushinda kwa wanaume.

https://p.dw.com/p/4QBiu
Symbolbild - Schach
Picha: Photology2000/Shotshop(picture alliance

"Sidhani kama jambo kama hilo limewahi kutokea popote duniani," alisema John Mukabi, katibu mkuu wa Shirikisho la Chess la Kenya. Mukabi alisema baada ya tapeli huyo kufichuliwa alieleza kuwa amefanya hivyo kwa sababu alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda zawadi ya shindano la wanawake.

Shindano la 31 la Kenya Open, ambalo ni la kimataifa la mchezo wa chess mjini Nairobi lililofanyika kuanzia Aprili 6-10, lilivutia washiriki 445, huku 84 wakishiriki katika mashindano ya wanawake. Mchezaji mmoja aliyefunika uso, mkimya na asiyeeleweka, alivutia mashaka yanayoongezeka kadiri raundi zilivyokuwa zikiendelea.

"Dokezo la kwanza kwamba kulikuwa na tatizo lilikuwa wakati nilipozunguka na mpiga picha kupiga picha za shindano hilo," Mukabi aliambia AFP siku ya Jumapili.

"Tuliporudi kwenye kompyuta kuweka majina, jina lilikuwa Milicent Awour. Tulitarajia jina la Kiislamu. Ilikuwa ni jambo lisilo la kawaida lakini inawezekana kwamba kuna watu wenye majina ya Kikristo ambao ni Waislamu." Alisema wasimamizi wa mechi pia wanazua shaka.

BG Schach-WM 1972 | signiertes Schachbrett der WM
Kijana mwanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi Milicent Awour alijivisha niqab na kushiriki mashindano ya wanawake ili kushinda zawaid ya pesa kwa urahisi.Picha: AP/picture alliance

"Waamuzi pia waligundua kitu: baada ya michezo, mtu huyu anatoweka na anarudi tu na dakika chache kabla ya kuanza kwa mzunguko unaofuata," Mukabi alisema.

"Kuna mtu pia aliona kwamba mabega yalionekana ya kiume zaidi kuliko ya kike... Hata viatu vya raba alivyokuwa amevaa, vilihusishwa zaidi na wanaume." Mshindani huyo wa siri pia alikuwa akipata matokeo mazuri.

"Jambo lingine ni kwamba alikuwa amemshinda mwanadada mzoefu sana, ambaye alishiriki mara sita katika Olympiad ya Dunia ya Chess kwa Kenya," alisema Mukabi.

Baada ya raundi ya nne, maafisa walichukuwa hatua. Ilikuwa checkmate katika moja.

"Baada ya mchezo huo waamuzi walimchukua kando na msuluhishi mmoja wa kike alikwenda naye kwenye vyumba vya kuogea ambako alitakiwa kuvua hijabu, alipofika huko mara moja alikiri kuwa yeye ni mwanamume, akatolewa na alama zikabadilika."

"Alisema matatizo ya kifedha yalimfanya afanye hivyo,” alisema Mukabi. "Katika kitengo cha wanaume, hakuwa na nafasi kabisa, tulikuwa na Grand Masters Mkuu, Masters wa Kimataifa..."

Kijana huyo ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anatazamiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya shirikisho la mchezo wa chess nchini Kenya wiki ijayo. Anakabiliwa na kusimamishwa kwa miaka kadhaa.

Chanzo: AFPE