1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa wa upinzani Rwanda auawa

25 Septemba 2019

Shirika la Amnesty International limeelezea masikitiko yake kufuatia kuuawa kwa mwanasiasa wa upinzani wa Rwanda Syldio Dusabumuremyi wa chama cha FDU-Inkingi kinachoongozwa na Victoire Ingabire.

https://p.dw.com/p/3QDbj
Logo Amnesty International

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeelezea kushtushwa na kifo cha mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Syldio Dusabumuremyi ambaye alipatikana amekufa katika wilaya ya Muhanga kusini mwa nchi hiyo. 

Syldio Dusabumuremyi ambaye ni afisa mwenye ushawishi wa chama cha upinzani nchini Rwanda FDU-Inkingi, alidungwa kisu hadi kufa usiku wa kuamkia Jumanne. Kiongozi wa chama hicho Victoire Ingabire ameutaja mkasa huo kama jaribio la kuwatishia wapinzani wa serikali.

Hapo jana, maafisa wa polisi wa Rwanda walithibitisha kuwa Syldio Dusabumuremyi mwenye umri wa miaka 42, aliuawa usiku wa kuamkia Jumanne na kwamba tayari washukiwa wawili wametiwa mbaroni.

Kwenye taarifa, mkurugenzi wa shirika la Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki Joan Nyanyuki amesema mauaji ya kikatili ya Syldio Dusabumuremyi yanashtusha mno.

Nyanyuki ameendelea kusema kuwa kifo hicho kinatatiza zaidi ikizingatiwa kimejiri baada ya misururu ya mashambulizi yenye mashaka.  Ametaka kukomeshwa kwa hali ya sasa ya wanasiasa wa upinzani kutishwa na kuhangaishwa.

Victoire Ingabire, kiongozi wa chama cha upinzani FDU-Inkingi nchini Rwanda
Victoire Ingabire, kiongozi wa chama cha upinzani FDU-Inkingi nchini RwandaPicha: Reuters/J. Bizimana

Serikali ya Rwanda yahimizwa kuheshimu haki na uhuru

Amnesty International imeongeza kuwa ni muhimu kwa serikali ya Rwanda kulinda na kuheshimu haki na uhuru wa kujieleza na kukusanyika ikiwemo kwa wanasiasa wa upinzani.

Victoire Ingabire ambaye anakiongoza chama cha FDU-Inkingi, ambacho kimekuwa kikimpinga Rais Paul Kagame tangu mwaka 2000, amesema Dusabumuremyi alikuwa mratibu wa kitaifa wa chama chake na anaamini kifo chake kimechochewa kisiasa.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters jana alipofika mahakamani kusikiliza kesi inayowaandama maafisa wake tisa wanaokabiliwa na mashtaka yanayofungamana na ugaidi, Ingabire amedai kuwa watu ambao hakuwataja majina wanatumia mbinu hizo kwa lengo la kumzuia asiunde chama cha upinzani

Ingabire pamoja na Amnesty International wametoa orodha ya wanasiasa wa upinzani nchini Rwanda ambao wameuawa au wametoweka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Imago/Zumapress/M. Brochstein

Visa vya mauaji ya kutatanisha na watu kutoweka

Marehemu Dusabumuremyi ni msaidizi wa pili wa Ingabire kuuawa mwaka huu. Mnamo mwezi Machi, msemaji wa Ingabire pia alipatikana amefariki. Aidha katika mwaka huu, maafisa wengine wawili wa Ingabire wametoweka kwa njia za kutatanisha.

Ingabire aliliambia shirika la habari la Ujerumani DPA kwamba ikiwa rais wa Rwanda Paul Kagame anafahari kuhusu usalama wa nchi hiyo, basi inampasa kuelewa kwamba wanachama wa upinzani pia ni miongoni mwa idadi jumla ya raia wa nchi hiyo.

Ingabire alifungwa jela miaka minane kwa kutishia usalama na kile kilichotajwa kuwa kuyadunisha mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini humo, ambapo zaidi ya watu 800,000 waliuawa.

Awali, Ingabire aliwahi kusema kuwa hata kesi dhidi yake pia ilichochewa kisiasa. Alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Kagame ambaye japo anasifiwa kwa kusaidia katika ukuaji na uimarishaji wa uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, pia wanaharakati wanadai anakandamiza haki za binadamu na kuminya uhuru wa vyombo vya habari na wa wanasiasa. Madai ambayo Rais Kagame huyakanusha mara kwa mara.

Vyanzo: RTRE, DPAE