1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamgambo wetu ndiye aliyelipua Manchester: IS

23 Mei 2017

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu linasema mmoja wa wanachama wake ndiye aliyejilipua katikati ya kundi la watu waliokuwa wanahudhuria tamasha la muziki la mwanamuziki kutoka Marekani Ariana Grande, usiku wa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/2dSdx
Großbritannien Polizeieinsatz nach Explosion in Manchester
Polisi wakilinda usalama katika eneo la tukio huko ManchesterPicha: Getty Images/AFP/P. Ellis

Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 22 na kuwajeruhi wengine 59. Polisi nchini Uingereza lakini wamesema kwamba ni kilipuzi cha kujitengenezea tu kilichotumika katika shambulizi hilo.

Magaidi hao wanaojiita Dola la Kiislamu wanasema mwanamgambo wao alitega bomu katikati ya watu waliokuwa katika tamasha hilo kisha kulilipua bomu hilo, ingawa hawakusema iwapo mwanamgambo huyo alifariki. Kundi hilo linazidi kusema watu 30 ndio waliouwawa na majeruhi ni 70, idadi hiyo ikiwa ni ya juu ikilinganishwa na ile iliyotolewa na serikali ya Manchester, inayosema pia aliyefanya shambulizi hilo alifariki dunia.

Polisi mjini Manchester imesema imemkamata mtu mmoja mwenye umri wa miaka 23 kuhusiana na shambulizi hilo kusini mwa Manchester, saa chache baada ya tukio, ingawa hawajatoa taarifa zaidi kuhusiana na mtu huyo. Polisi pia imesema kuna mtu mwengine aliyetiwa nguvuni na maafisa katikati mwa mji huo ingawa haijulikani iwapo kukamatwa kwake kunahusiana na shambulizi hilo.

G7 itatuma ujumbe mzito kwa ugaidi

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema polisi inamfahamu aliyefanya shambulizi hilo na kwamba serikali itawapa ushirikiano katika uchunguzi wanaoufanya kwa sasa.

Großbritannien PK Theresa May zum Anschlag in Manchester
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/T. Melville

"Polisi na mashirika yanayotoa huduma za usalama watapewa raslimali zote wanazohitaji kukamilisha uchunguzi wao," alisema May. "Polisi wanaamini wanamjua aliyefanya shambulizi hilo lakini katika hatua hii ya uchunguzi wao, hatuwezi kuthibitisha jina lake."

Waziri Mkuu wa Italia Paolo Gentiloni akizungumza na wanahabari mjini Roma Jumanne, alisema mkutano mkuu wa mataifa saba yenye ushawishi mkubwa wa kiuchumi G7 utakaoandaliwa mjini Sicily wiki hii, utazaa maazimio yatakayohakikisha kwamba mataifa hayo yamejitolea katika kupambana na ugaidi.

"Tunashirikiana kwa sasa kuhakikisha kwamba tunatuma ujumbe mzito dhidi ya ugaidi kutoka G7. Tutakuwa na fursa ya kuyazungumzia tena upya na kwa pamoja katika mkutano huo," alisema Gentiloni, "kwamba matukio ya kuwashambulia na kupoteza maisha ya vijana, hayatoushinda uhuru wetu."

Ulaya imeshambuliwa sana katika miaka miwili iliyopita

Shambulizi hilo la Manchester limeyafanya mataifa mengine Ulaya kuwa makini zaidi na usalama wake kwani waziri wa usalama wa ndani wa Ufaransa Gerard Collomb alisema, serikali ya nchi hiyo itatoa maagizo kwa waandalizi wa matamasha ya jinsi ya kuyaweka salama maeneo wanayoandaa matamasha yao.

Portugal Papst Johannes in Fatima
Papa Francis pia ametoa rambi rambi zakePicha: picture-alliance/NurPhoto/P. Fiuza

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis, alituma ujumbe wa kuelezea kusikitishwa kwake na tukio hilo na akawapongeza polisi na waliotoa huduma za dharura kwa juhudi zao za kuwaokoa watu.

Shambulio hili la Manchester ni la karibuni kabisa  miongoni mwa mashambulizi ambayo yamelenga sehemu tofauti Ulaya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Miongoni mwa mashambulizi hayo ni lile la Brussels la Machi 22 mwaka 2016 ambapo watu 32 waliuwawa na mwezi Desemba mwaka jana watu 12 waliuwawa mjini Berlin baada ya jamaa mmoja kuendesha lori kwenye soko la Krismasi.

Ufaransa ndiyo iliyoathirika zaidi na matukio haya ya kigaidi miongoni mwa mataifa ya Umoja wa Ulaya, kwani jumla ya watu 238 wamepoteza maisha katika kipindi hicho cha miaka miwili.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman