1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yaadhimisha mwaka mmoja wa mapinduzi ya kijeshi

1 Februari 2022

Wapinzani wa utawala wa kijeshi nchini Myanmar wameadhimisha mwaka mmoja wa mapinduzi ya kijeshi nchini humo kwa mgomo wa kitaifa kuonyesha mshikamano wao, huku jeshi likiendelea kung'ang'ania madaraka

https://p.dw.com/p/46M6f
Myanmar | Protest
Picha: AP Photo/picture alliance

Mgomo huo wa kimya kimya ulinuia kuwafanya watu kubaki majumbani na kufunga biashara zao kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni. Huko Yangon, jiji kubwa zaidi nchini humo na kwingineko, picha zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii zilionesha barabara ambazo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi zikiwa na watu wachache mno.

Siku ya Jumatatu raia nchini Myanmar walikimbilia kununua bidhaa muhimu kabla ya kuanza kwa mgomo huo. Shirika la habari la serikali limeripoti kuwa jana kiongozi wa kijeshi Min Aung Hlaing, aliongeza muda wa hali ya hatari iliyotangazwa wakati wa mapinduzi hayo kwa miezi sita kuwezesha kufanywa kwa uchaguzi ulioahidiwa huku kukiwa na vitisho vya ndani na nje  na mashambulizi ya kigaidi pamoja na uharibifu.

Gazeti la serikali la Myanmar Alin, limeripoti kuwa mamlaka ya kijeshi pia ilijaribu kutibua maandamano hayo ya Jumanne kwa kuwakamata watu 70 katika muda wa siku tatu zilizopita kwa kuchochea maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii.
Wamiliki wa biashara pia walionywa kwamba mali zao zitazuiwa iwapo watashiriki katika mgomo huo. Waandamanaji pia huenda wakakabiliwa na vifungo vya muda mrefu gerezani.

Aung San Suu Kyi
Aung San Suu Kyi - Kiongozi wa Myanmar aliyeondolewa madarakaniPicha: Aung Shine Oo/AP Photo/picture alliance

Maadhimisho hayo pia yamevutia hisia za kimataifa, hasa kutoka mataifa ya Magharibi yanayokosoa mapinduzi hayo ya kijeshi kama vile Marekani. Katika taarifa yake, rais wa Marekani Joe Biden  alitoa wito kwa jeshi kubadili vitendo vyake, kumwachilia huru kiongozi wa kiraia aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi na wafungwa wengine na kushiriki katika mazungumzo ya maana ya kuirejesha Myanmar kwenye njia ya demokrasia.

Siku ya Jumatatu, Marekani iliweka vikwazo vipya kwa maafisa wa Myanmar kuongezea kwa vile ambavyo tayari vimewekewa maafisa wakuu wa jeshi.  Marekani, imezuia mali yoyote ambayo waliolengwa wanamiliki nchini humo na kuwazuia raia wake kufanya biashara na walengwa hao. Uingereza na Canada pia zimetangaza hatua kama hizo. Taarifa kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, imeangazia kuongezeka kwa ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu, mizozo na kasi ya umaskini nchini Myanmar, hali aliyosema inahitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Gazeti la The Global New Light of Myanmar limeripoti kuwa serikali hiyo ya kijeshi  itajitahidi kufanya uchaguzi mpya pindi hali itakaporejea kuwa tulivu na ya amani. Awali jeshi lilikuwa limeahidi kuandaa uchaguzi ndani ya miaka miwili lakini mwezi uliopita, msemaji wake akasema kuwa uchaguzi huo sasa umepangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2023.