1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa Ujerumani na Ufaransa wahujumu hatua za EU

26 Oktoba 2022

Uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa upo matatani tena, wakati huu ukionekana kuwa mbaya kuliko awali. Mvutano huu unajiri pia wakati mbaya kwani unahujumu uwezo wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua dhidi ya migogoro iliyopo.

https://p.dw.com/p/4IgQN
Deutschland Frankreichs Präsident Macron trifft Bundeskanzler Scholz in Berlin
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Tangazo la hivi karibuni kwamba mkutano wa mawaziri wa Ujerumani na Ufaransa unaahirishwa hadi mwezi Januari, linaonekana kufichua mzozo uliopo kati ya mataifa hayo mawili.

Mara nyingi ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa hutajwa kuwa injini ya Umoja wa Ulaya. Lakini wachambuzi wanasema mvutano wa sasa unahujumu uwezo wa umoja huo kuchukua hatua.

Ikulu ya rais nchini Ufaransa hata hivyo ilisema mkutano huo umeahirishwa kwa sababu ya changamoto za ratiba za mawaziri wengi na vilevile ukosefu wa muda kuuandaa mkutano huo.

Mpango wa gesi wa Ujerumani wasababisha mgawanyiko Ulaya kuhusu nishati

Na kwamba kucheleweshwa kwake si ishara ya kuwepo mvutano baina ya nchi hizo na kuongeza kuwa mkutano umeahirishwa tu wala haujafutwa.

Hata hivyo taarifa hiyo ya msemaji wa ikulu ya rais Ufaransa, pamoja na ziara ambayo imepangwa kwa haraka ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz Jumatano hii kuelekea Ufaransa, hazikuwashawishi wachambuzi.

Stefan Seindorf, ambaye ni naibu mkurugenzi wa taasisi ya wachambuzi wa ushirikiano wa Ujerumani na Ufaransa DFI, amesema kwa ujumla mkutano wa mawaziri wa mataifa hayo mawili hautoi matokeo mengi muhimu na madhubuti isipokuwa nafasi ya kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wao.

Ushirikiano mzuri wa Ujerumani na Ufaransa hutizamwa kuwa injini ya Umoja wa Ulaya unaofanya kazi.
Ushirikiano mzuri wa Ujerumani na Ufaransa hutizamwa kuwa injini ya Umoja wa Ulaya unaofanya kazi.Picha: Yves Herman/REUTERS

Hata hivyo Seindorf amesisitiza kuwa mikutano hiyo ni muhimu kwa Umoja wa Ulaya kufanya kazi. Ameliambia shirika la habari la DW kwamba hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huo wa mawaziri kufutwa tangu mwaka 1963.

Je kila nchi inataka kufanya mambo yake kivyake?

Hivi karibuni, Ujerumani ilipitisha bila ya kuifahamisha Ufaransa, mpango wake wa dharura wa euro bilioni 200 kusaidia raia wake dhidi ya ongezeko la bei ya nishati. Wadadisi wanasema ingekuwa heshima ya kawaida kuifahamisha Ufaransa kwani kitita kama hicho kinaweza kushawishi soko.

Katika kisa kingine wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Ujerumani ilisaini makubaliano na nchi nyingine 14 za NATO kuhusu mfumo mpya wa ulinzi wa anga uitwao Sky Shield Initiative au ESSI.

Mpango huo unalenga kuunda mfumo wa ulinzi wa angani wa pamoja barani Ulaya. Lakini Ufaransa haikujumuishwa.

Hii ni licha kwamba tayari Ufaransa inatengeneza mfumo wa ulinzi wa angani dhidi ya makombora kwa jina Mamba ikishirikiana na Italia.

Kwa upande mwingine, wiki iliyopita wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza makubaliano kati ya nchi yake, Ureno na Uhispania ya kujenga bomba jipya la haidrojeni na gesi kati ya miji ya Barcelona na Merseille.

Tangu mwanzo wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari mwaka huu, ulinzi wa kijeshi umepewa umuhimu mkubwa.
Tangu mwanzo wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari mwaka huu, ulinzi wa kijeshi umepewa umuhimu mkubwa.Picha: Robin Van Lonkhuijsen/ANP/dpa/picture alliance

Mradi huo unauzima kabisa ule uliopendelewa na Ujerumani wa Midcat ambao ungeunganisha Uhispania na Ufaransa kupitia milima ya Pyrenees. Ujerumani ilikuwa na matumaini kuwa ingenufaiika na gesi ya mradi huo.

Rais wa Ufaransa pia aliikosoa Ujerumani aliposema, si vyema kwa Ujerumani wala kwa Ulaya, ikiwa Ujerumani inajitenga.

Kulingana na Seidendorf, pande zote zinaudhi.

Mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa amehoji kuwa Ujerumani inaonekana kudhani kwamba inaweza kusaini makubaliano mengi na nchi nyingine ndogo na iiache Ufaransa nje. Nayo Ufaranya ingali inasubiri Ujerumani kuridhia ahadi ya utangamano zaidi ndani ya Umoja wa Ulaya ambayo iliyotolewa na Macron mwaka 2017.

Sophie Pornschlegel, mchambuzi wa ngazi ya juu wa sera katika taasisi iliyoko Brussels, ameliambia DW kwamba muda haupo kuruhusu mivutano baina ya nchi hizo hasa wakati huu ambapo kuna vita Ukraine na vilevile mgogoro wa nishati

Amesisitiza kuwa mpasuko kati ya Ujerumani na Ufaransa ndio rais wa Urusi Vladimir Putin anapenda na inahujumu uwezo wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua.

(DW)

Mwandishi: Lisa Louis

Tafsriri: John Juma