1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa Uhispania bado waendelea

19 Oktoba 2017

Kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont atishia kutangaza uhuru wa jimbo lake ikiwa hakutokuwepo na mazungumzo. Serikali ya Uhispania imesema itatumia kifungu cha katiba kufuta mamlaka ya ndani ya jimbo la Catalonia.

https://p.dw.com/p/2mA4l
Spanien Carles Puigdemont Premier der Regionalregierung
Picha: Reuters/I. Alvarado

Kiongozi huyo wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont amemwandikia barua waziri mkuu wa Hispania Mariano Rajoy saa chache kabla ya kumalizika muda aliopewa wa kuahirisha jitihada zake za kutaka kutangaza uhuru wa Catalonia.  Serikali ya Uhispania imesema waziri mkuu Mariano Rajoy atafanya mkutano maalumu wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuzindua mchakato wa kuchukua baadhi ya udhibiti kamili wa mamlaka ya ndani ya jimbo la Catalonia. Hayo ni majibu ya serikali ya Uhispania kutokana na barua iliyoandikwa na rais wa Catalonia Carles Puigdemont.

Serikali kuu ya Madrid imeahidi kuainisha Kifungu cha 155 na kusimamisha mamlaka ya jimbo la Catalonia ikiwa Puigdemont hatotoa majibu yenye kuridhisha na kutamka kuwa hatatangaza uhuru wa jimbo hilo.  Serikali ya Uhispania imekataa kufanya mazungumzo hadi pale kiongozi huyo wa jimbo la Catalonia  atakapoyaacha madai yake ya kutaka kulitenga jimbo la kutoka Uhispania. Waziri mkuu Mariano Rajoy ametoa mwito kwamba juhudi zifanyike kumshawishi Puigdemont aache kusababisha matatizo zaidi yatakayoilazimisha serikali ichukue hatua ambazo si lazima zichukuliwe.Serikali ya Uhispania ilitegemea jawabu kufikia muda wa saa nne na nusu leo asubuhi.

Spanien Premierminister Mariano Rajoy
Waziri mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Reuters/M. Vidal

Utawala wa jimbo la Catalonia na serikali kuu ya Uhispania zimekuwa zikivutana katika mgogoro wa kikatiba tangu Puigdemont alipotangaza kuwa jimbo hilo lina mamlaka ya kuwa na uhuru hapo tarehe10 mwezi Oktoba tamko ambalo aliliahirisha muda mfupi baadaye. Puigdemont pia alishindwa mnamo tarehe 16 Oktoba kutoa jibu la ndiyo au hapana kwa mamlaka ya mjni Madrid pale alipotakiwa kufafanua iwapo ametangaza uhuru wa Catalonia au la.

Taarifa ya leo ni nafasi ya pili na ya mwisho iliyowekwa na serikali kuu kabla ya haijatekeleza Kifungu cha 155 cha Katiba ya Uhispania kilichopitishwa mwaka 1978, ambayo inaweza kusitisha uhuru wa jimbo la Catalonia na kuweka mazingira ya kufanyika uchaguzi mpya.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/dw.com/p/2m92R

Mhariri:Josephat Charo