1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya waislamu na serikali Burundi waongezeka

9 Juni 2021

Hali ya kutoelewana inazidi kuongezeka kati ya waislamu na wizara ya mambo ya ndani Burundi, baada ya Sheikh Rashidi Ndikumana kukamatwa baada ya kumtaka waziri Ndirakobuc kuwaomba radhi waislam, kufuatia tamko lake

https://p.dw.com/p/3udEi
Burundi Gitega | Beerdigung des ehemaligen Präsidenten Pierre Nkurunziza: Evariste Ndayishimiye hält Ansprache
Picha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Sheikh Rashid Ndikumana mmoja ya masheikh wakuu nchini humo  amekamatwa na kutiwa nguvuni na polisi baada ya kudaiwa kumjibu waziri wa mambo ya ndani, maendeleo ya jamii na usalama Gervais Ndirakobuca, juu ya matamshi aliyoyatoa kuhusiana na Adhana ama wito wa kuwataka waislam kudiriki sala.

Tukio la kukamatwa sheikh Rashid lilizusha vuta nikuvute kati ya poilisi na baadhi ya waumini katika mtaa wa Buterere kusini mwa jiji la Bujumbura ambako sheikh huyo anaishi na pia anaongoza masjid Madina.

Sheikh huyo alimtaka waziri mambo ya Ndani kutambuwa kuwa adhana katika uislamu ilikuwepo kabla ya kuzaliwa kwake na utaendelea kuwepo. Hata Hivyo alimuagiza kuwataka radhi waislam katika kipindi kisichozidi wiki moja la sivyo watamuomba Rais Evariste Ndayishimiye kumfuta kazi.

Waziri Gervais Ndirakobuca katika mkutano na viongozi wa dini mbalimbali zinazopatikana nchini, alibani kuwa raia wanakerwa na kelele za makanisa na adhana. Na kwamba haieleweki adhana saa za alfajiri ni kero kwa raia kwani ni jukumu kwa muumini kujua wakati wake wa kusali pasina kusikika adhana.

''Hakika raia wamechoshwa, ni hali ya kutokubalika. Kumekuwa na ujenzi kiholela wa misikiti, hata sehemu ambako hakuna muumini hata mmoja wa dini ya kiislam utakuta kunajengwa msikiti. Vipaza sauti saa tisa za usiku, sidhani kuwa kuna mtu anayesikiliza. Mtu anayejua ni muumini na jukumu lake kwenda kusali pasina kuamshwa kwa vipaza sauti,'' alisema Waziri Ndirakobuca.

Matamshi hayo yamezusha hasira kwa waislam wengi nchini. Sauti zilojaa hasira zimetanda kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa waislam wa ndani na nje ya nchi wakizungumzia thamani ya adhana katika uislam huku wengine wakimtaka waziri kuiomba radhi jamii. Huku wengine wakisambaza adhana.

Hali hiyo imejitokeza wakati kulikuwepo na mvutano mwingine kufuatia waziri wa mambo ya ndani kumsimamisha kiongozi aliyechaguliza na waislam, Hassan Nyamweru na kumuweka kiongozi wa mpito ambaye ni Iddi Kabano aliyetajwa kuwa mfuasi wa chama tawala.

Mwandishi:  Amida ISSA, DW-Bujumbura