1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Upinzani Zimbabwe wapinga ushindi wa Rais Mnangagwa

28 Agosti 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa jana amepinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa.

https://p.dw.com/p/4VdGa
Mgombea urais wa muungano wa CCC Nelson Chamisa
Mgombea urais wa muungano wa CCC Nelson ChamisaPicha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP Photo/picture alliance

Nelson Chamisa badala yake amedai ushindi katika uchaguzi ambao waangalizi wa kimataifa wameuelezea kuwa, haukukidhi viwango vya kidemokrasia.

Muungano wa upinzani wa wananchi kwa ajili ya mabadiliko CCC ulikataa matokeo ya uchaguzi huo na kudai yalikuwa matokeo ya "uongo."

Chamisa, wakili na mchungaji wa kanisa amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Harare kuwa, muungano wa CCC ndio ulioshinda uchaguzi huo na anashangaa kwanini Mnangagwa ametangazwa mshindi.

Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa mnamo siku ya Jumamosi na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ZEC, Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80, alishinda muhula wa pili wa urais kwa kupata asilimia 52.6 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Chamisa aliyejizolea asilimia 44 ya kura zote zilizopigwa.

Raia wa Zimbabwe walipiga kura ya urais na bunge siku ya Jumatano na Alhamisi, katika uchaguzi uliogubikwa na madai ya wizi wa kura, kukandamizwa kwa wapiga kura na kucheleweshwa kwa zoezi la kupiga kura katika baadhi ya wadi.