1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Scholz umepata pigo uchaguzi wa bunge la Ulaya

10 Juni 2024

Matokeo ya awali ya bunge la Ulaya yanaonesha muungano wa Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz umeshindwa vibaya ambapo vyama vyote vitatu katika serikali yake vimekuwa nyuma ya vile vya kihafidhina na mrengo mkali wa kulia.

https://p.dw.com/p/4gqqF
Uchaguzi wa Ulaya Potsdam Kansela Scholz
Olaf Scholz, Kansela wa Shirikisho la Ujerumani, akipiga kura yake katika kituo cha kupigia kura huko Potsdam, Ujerumani 09 06 2024 Picha: Janine Schmitz/photothek/IMAGO

Matokeo hayo yanaibua wito kutoka kwa vyama vya upinzani vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union, CSU viliyoshinda kwa Scholz wa mrengo wa kati kubadili mkondo au kuandaa uelekeo kwa uchaguzi mpya.

Upinzani unaongeza shinikizo ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi muhimu wa kikanda katika majimbo kadhaa ya mashariki ambapo chama cha mrengo wa kulia kinatabiriwa kuibuka na ushindi.

Matokeo mabaya zaidi kwa kihistoria ya chama cha Social Democrats (SPD)

Chama cha Social Democrats (SPD) cha Scholz kimepata matokeo mabaya zaidi katika historia kwa asilimia 14, kikiwa cha tatu nyuma ya  chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deustchland (AfD) kilichopata karibu asilimia 16, na nyuma pia ya kambi ya kihafidhina ya CDU-CSU kwa asilimia 30.

Washirika wa muungano wa SPD, walinzi wa mazingira-The Greens wamepata asilimia 12 huku chama cha kiliberali cha FDP kikipata asilimia tano.

Katibu mkuu wa CDU Carsten Linnemann amesema Scholz anapaswa kuitisha "kura ya imani" kufuatia matokeo mabaya. Muungano lazima ubadilishe mkondo "au ufungue njia ya uchaguzi mpya," alisema Linnemann.

Makao na ulinganifu wa sauti ya wapiga kura wa Ujerumani

Uchaguzi wa bunge la Ulaya 2024 | Mabango ya uchaguzi Ujerumani
Mabango ya wagombea mbalimbali nchini Ujerumani kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika Juni 9 katika mataifa tofauti ya Ulaya.Picha: Goldmann/picture alliance

Gazeti la kila siku lenye wasomaji wengi la Ujerumani la Bild limeandika "Wapiga kura wametuma ujumbe wa wazi kwa muungano huo kubadilisha kwa kiasi kikubwa siasa zake hasa katika  uhamiaji, uchumi na ulinzi wa mazingira."

Serikali ya pande tatu ya Scholz imekuwa ikikabiliana na mfululizo wa mizozotangu ilipochukua mamlaka Desemba 2021, baada ya chama chake cha SPD kuwashinda wahafidhina wa kansela wa zamani Angela Merkel. Miezi michache tu baada ya kuanza kazi ililazimika kukabiliana na uvamizi wa Urusi kwa Ukraine na mzozo wa nishati ulioitumbukiza Ujerumani kwenye mdororo wa kiuchumi.

Uchumi unanawiri katika hali dhaifu

Kutoridhika kwa wapiga kura kunasalia kuwa katika hali ya juu kwa masuala ya sheria za  mabadiliko ya tabia nchi hadi kupunguza matumizi, wakati uhalifu na uhamiaji unasalia kuwa  wasiwasi kwa umma. Chama cha walinzi wa mazingira-The Greens, haswa kimepata pigo juu ya mipango ya kuibadili Ujerumani kwa matumizi nishati mbadala ambayo inahitaji gharama kubwa katika uwekezaji.

Maoni ya umma pia yanasalia kugawanyika kuhusu jinsi muungano wa Scholz ulivyoshughulikia vita vya Ukraine, huku baadhi yao wakiwa nyuma ya uamuzi wake wa kutoa silaha kwa Kyiv na wengine wakihofia uungwaji mkono huo ungeiingiza Ujerumani vitani.

Soma zaidi:Wapiga kura wahitimisha uchaguzi wa bunge la Ulaya

Matokeo ya AfD yanaashiria kupanuka kwa wigo wa ushawishi wake tangu mwaka 2019, pale ilipopata asilimia 11. Chama hicho kililazimika kumpiga marufuku mgombea wake mkuu Maximilian Krah kufanya kampeni kwa sababu anachunguzwa kwa uhusiano unaotiliwa shaka dhidi ya Urusi na Uchina.

Chanzo: AFP