1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni atofautiana na mahakama kuhusu dhamana kwa wafungwa

28 Septemba 2021

Rais Yoweri Museveni wa Uganda anataka washukiwa wa mauaji na makosa mengine makubwa kama uhaini wasipewe dhamana lakini jaji mkuu ametahadharisha kuwa mabadiliko hayo yanakinzana na utawala wa sheria na haki za binadamu

https://p.dw.com/p/40yVV
Uganda Wahl 2021 | Yoweri Museveni, Präsident
Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Kwa muda wa miaka 10 sasa, rais Museveni amekuwa akikariri mtazamo wake kuwa washukiwa katika hatia za mauaji, uhaini, ubakaji na unajisi wasipewe dhamana hata kidogo. Amefufua tena mjadala huo siku ya Jumatatu alipoongoza sherehe za kumbukumbu za marehemu jaji mkuu Benedicto Kiwanuka aliyeuawa katika utawala wa Iddi Amin akisema kuwa jamii huona kero kubwa kuona mtu ambaye anashukiwa kutenda mauaji akiwa huru huku kesi dhidi yake ikiendeshwa kwa muda mrefu.

Rais alikuwa akimjibu jaji mkuu kwenye sherehe hizo aliyesisitiza kuwa kamwe kitengo cha sheria hakiwezi kusaliti katiba ya nchi kwa kuwanyima dhamana washukiwa kama anavyopendekeza yeye.

Jumuiya ya wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wameendelea kupinga wazo la Museveni kwamba sheria zifanyiwe mageuzi dhamana ya mahakama kwa wanaoshukiwa kutenda uhalifu wa hali ya juu wasiachiwe.

Wameunga mkono jaji mkuu Alphose Owiny-Dollo kwa kumwambia waziwazi rais Museveni ambaye ndiye alimteua kuhusu msimamo wa kitengo cha sheria ambacho ni moja kati ya mihimili mitatu ya serikali mingine ikiwa bunge na baraza la mawaziri.

Wanasheria wasema Museveni anataka kufanya mageuzi ili azidi kuukandamiza upinzani

Weltspiegel 16.03.2021 | Uganda Kampala | Verhaftung Bobi Wine, Politiker
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Wanasheria wana  mtazamo kuwa kwa mara nyingine rais anajaribu kuifanyia mageuzi katiba na kuzidi kukandamiza wapinzani wake akitumia sheria.

Katika kile kinachochukuliwa na wengi kuwa vyombo vya dola tayari vinafuata na kutekeleza wazo la amiri mkuu wa majeshi Jenerali Yoweri Museveni, hapo jana askari walinaswa hadharani wakimkamata mbunge Muhamad Segirinya hatua chache kutoka katika gereza la Kigo alikoachiwa kwa agizo la mahakama baada ya mawawikili wake kuomba dhamana.

Mbunge huyo na mwenzake Allan Sewanyana wanakabiliwa na madai ya kupanga na kutekeleza mauaji ya raia katika eneo la Greater Masaka.

Wakati huohuo, akiwa mwenyekiti wa chama tawala cha NRM, Museveni ameitisha mkutano wa dharura wa wabunge wa chama hicho.

Wadadisi wa kisiasa wanabashiri kuwa anawataka kuunga mkono muswaada wa kuifanyia katiba mageuzi ili sheria ya dhamana ifanyiwe mabadiliko kama anavyopenda yeye.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala