1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muafrika Kusini Patrice Motsepe achaguliwa rais wa CAF

12 Machi 2021

Mgombea pekee Patrice Motsepe amethibitishwa kuwa rais mpya wa shirikisho la kandanda barani Afrika mjini Rabat Ijumaa, na kuomba umoja wakati akitafuta kurejesha sifa ya shirika hilo.

https://p.dw.com/p/3qZjF
Fußbal | Caf - Dr Patrice Motsepe
Picha: Muzi Ntombela/BackpagePix/empics/picture alliance

"Afrika inahitaji busara za pamoja, lakini pia kipaji cha kipekee na busara za kila rais wa chama cha soka na kila taifa mwanachama," Motsepe alisema.

"Tukifanya kazi pamoja, soka barani Afrika itashuhudia mafanikio na ukuaji ambavyo haijavifaidi katika kipindi kilichopita."

Motsepe alisema kulikuwa na "hisia za uharaka wa juu" ili "kuweka sawa nafasi ya kifedha ya CAF". Hata hivyo, aliweka msisitizo pia kwenye kuboresha ufanisi wa timu za Afrika kwenye ngazi ya kimataifa.

Bara hilo limekabiliwa na vizuizi katika miaka ya karibuni ambapo timu zote zilizofuzu kushiriki mashindano ya kombe la dunia 2018 nchini Urusi yaliondolewa kwenye raundi ya makundi.

Afrika Fußball Ahmad Ahmad
Rais wa zamani wa CAF Ahmad Ahmad kutoka Madagascar alipigwa marufuku na FIFA kujihusisha na mpira wa miguu kwa miaka miwili. Picha: FADEL SENNA/AFP via Getty Images

Soma pia: CAF: Soka ya Afrika katika njiapanda

"Mpira wa miguu ni zana yenye nguvu ya kurejesha fahari, heshima na taadhima ya Waafrika, na Afrika inaweza kutoa na kushindana kwa ngazi ya juu kabisaa duniani, katika mashindano yote - ya kombe la dunia na hata ubingwa wa vilabu wa FIFA," alisema katika hotuba yake.          

Alisema "dunia itatuheshimu tu" wakati timu za Afrika zitakapofanikiwa kimataifa. "Siyo wakati wachezaji wetu bora wanaheshimiwa barani Ulaya - Samuel Eto'o, Didier Drogba, Salah, Mane kutoka Liverpool, na George Weah. Tumelifanya hilo. Tunataka timu zetu za taifa kushindana na kushinda na kufanikiwa."

Motsepe anachukuwa hatamu za kuliongoza shirikisho linalokabiliwa na matatizo, baada ya Mmadagascar Ahmad Ahmad kuwa rais wa kwanza wa CAF kupigwa marufuku na FIFA Novemba mwaka jana, ambapo zuwio lake la kutojihuisha na soka kwa miaka mitano kuhusiana na "masuala ya utawala," limepunguzwa hadi miaka miwili baada ya kukata rufaa kwenye mahakama ya michezo.

Uingiliaji wa FIFA warahisha mchakato wa uchaguzi

Wiki chache tu zilizopita, Motsepe, raia wa Ivory Coast Jacques Anouma, Mmauritania Ahmed Yahya na Msenegali Augustin Senghor walikuwa wanapambania nafasi ya rais.

Afrika Fußball Jacques Anouma
Jacques Anouma ameteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa CAF.Picha: SIA KAMBOU/AFP via Getty Images

Lakini mikutano ya wagombea iliyoratibiwa na FIFA nchini Morocco na Mauritania ilipelekea Motsepe kuwa mgombea pekee. Senghor na Yahya walipewa nafasi za makamu wa kwanza na wa pili wa rais.

Anouma, ambaye awali aliyatangaza makubaliano hayo "kutokuwa ya kidemokrasia", ni mwanachama wa zamani wa kamati ya utendaji ya FIFA na anakuwa mshauri maalumu wa Motsepe.

Soma pia: CAF kupata uongozi mpya baada ya FIFA kuingilia kati

Wakati baadhi ya maafisa wa CAF wakilalamikia madai ya uingiliaji wa shirikisho la kimataifa, rais wa FIFA Gianni Infatino alipuuza jukumu la shirika lake.

"Nafurahi kwamba FIFA imeweza kuchangia, hata kama ni kidogo, juu ya wakati huu muhimu wa mpira wa miguu kwenye bara hili adhim," alisema.

Kocha mshindi wa zamani wa kombe la mataifa ya Afrika Claude le Roy alihoji ushiriki wa FIFA katika uchaguzi wa Motsepe, kwa kuzingatia kwamba "hawangethubutu kufanya hivyo barani Ulaya au Amerika Kusini".

"Infantino, acha mauaji na soka la Afrika ... kulaazimisha sheria yako kwa Afrika katika uchaguzi," Le Roy aliliambia shirika la habari la AFP.

FIFA Gianni Infantino und Ahmad Ahmad
Rais wa FIFA Gianni Infantino akiwa na rais wa CAF aliesimamishwa Ahmad Ahmad, Februari 2, 2018.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Bounhar

Maafisa wengi wanaamini Infantino tayari alimuunga mkono Ahmad kisiri miaka minne iliyopita, wakati Mmalagasy huyo alipokomesha uongozi wa miaka 29 wa Mcameroon Issa Hayatou.

Lakini baada ya mwanzo wa matumaini, Ahmad alianza kuboronga kuanzia mzozo mmoja hadi mweingine, ambayo hatimaye ilimsababishia kuondoka kwenye urais kwa fedheha.

"Shimo la rushwa na ubinafsi"     

FIFA iliingiwa na wasiwasi kuhusu masuala ya utawala ndani ya CAF kiasi kwamba ilimtuma katibu mkuu wake Fatma Samoura mjini Cairo kwa miezi sita kusaidia katika uendeshaji wa shirikisho hilo.

Motsepe ndiye tajiri wa tisa barani Afrika akiwa na utajiri binafasi unaokadiriwa na jarida la Forbes kufikia dola bilioni 2.9. Anamiliki klabu ya washindi ya Ligi ya mabingwa wa CAF mwaka 2015 ya Mamelodi Sundowns.

Anarithi shirika lililoelezwa kama "shimo la rushwa na ubinafsi" na gazeti la Afrika Kusini la Daily Maverick.

CAF-Präsident Issa Hayatou in Marokko
Issa Hayatou aliiongoza CAF kwa miaka 29 na utawala wake ulifikishwa kikomo na Ahmad Ahmad mwaka 2016.Picha: F. Senna/AFP/Getty Images

"CAF inahitaji vibaya kujitenga na njia za kizamani zilizochoka, tabia za kimfumo na hisia kwamba inawatumikia wale wanaokaa kwenye kamati ya utendaji, badala ya kinyume cha hilo," liliandika gazeti hilo.

CAF inamtegemea Motsepe kutumia mahusiano yake ya kibiashara barani Afrika kuvutia wafadhili wapya. Kampuni ya mafuta ya Ufaransa Total ndiyo wafadhali wakuu, lakini undani wa makubaliano ya miaka nane yalioanza 2016 haujawahi kuwekwa wazi.

"Asilimia 95 ya majadiliano yetu yatahusu soka..lakini nataka pia asilimia tano iwe kuhusu utambuzi kwamba soka haliwezi kufaniiwa na kustawi bila ushirikiano na sekta binafsi,W alisema Motsepe.

"Tunahitaji ushirika na sekta binafsi ili kufadhili na kuwezesha upatikanaji wa mapato zaidi."

Chanzo: AFPE