1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Mtoto wa rais wa zamani wa Niger aachiwa kwa dhamana

9 Januari 2024

Utawala wa kijeshi nchini Niger umemuachia huru mtoto wa Rais aliyepinduliwa madarakani Mohamed Bazoum.

https://p.dw.com/p/4b0K3
Rais wa Niger aliyepinduliwa Mohamed Bazoum
Rais Mohamed Bazoum aliyepinduliwa nchini Niger akiwa ziarani nchini Ufaransa:22.06.2023Picha: Stevens Tomas/ABACA/IMAGO

Kulingana na mahakama ya Kijeshi mjini Niamey, Salem Bazoum mwenye umri wa miaka 22 ameachiwa kwa muda Jumatatu jioni na atatakiwa kuwasili mahakamani ikiwa atahitajika.

Chanzo kilicho karibu na rais Bazoum kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba Salem Bazoum ameondoka Niamey kuelekea Lome, mji mkuu wa Togo, ambako aliwasili Jumatatu jioni.

Togo ni miongoni mwa mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi ambayo yamehusika katika upatanishi na utawala wa kijeshi wa Niger. Licha ya vikwazo mbalimbali, Togo imeendelea kuwa na  uhusiano wa karibu na Niger.

Kulingana na televisheni ya umma ya Niger, siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo Robert Dussey alikuwa ziarani mjini Niamey, ambako alikutana na waziri mkuu.

Rais Macron wa Ufaransa na Mohamed Bazoum wa Niger wakiwa mjini Paris
Rais aliyepinduliwa madarakani nchini Niger Mohamed Bazoum(kulia) akisalimiana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika Ikulu ya Elysée mjini Paris: 16.02.2023Picha: Michel Euler/AP/picture alliance

Tangu mapinduzi ya Julai 26 mwaka jana (2023), Niger inatawaliwa na viopngozi wa jeshi na Rais Bazoum na familia yake wanaendelea kuzuiliwa katika makazi ya rais.

Soma pia: Mawakili wa Bazoum wakanusha madai kwamba alijaribu kutoroka

Mapinduzi hayo yalilaaniwa kimataifa huku taifa hilo likikabiliwa na matatizo ya kiuchumi kufuatia vikwazo vya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).

Bei ya vyakula imepanda na kumeshuhudiwa uhaba wa bidhaa muhimu kama vile dawa, katika moja ya nchi maskini zaidi duniani.

Lakini mtawala wa kijeshi Jenerali Abdourahamane Tiani amesema ataongoza serikali ya mpito kwa muda wa miaka mitatu kabla ya kurejesha serikali ya kiraia.

Niger yaimarisha mahusiano na majirani zake

Niger | Jenerali Tiani aliyempindua rais Bazoum
Mtawala wa kijeshi wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani akilihutubia taifa Julai 28,2023 siku mbili baada ya mapinduziPicha: ORTN/Télé Sahel/AFP/Getty Images

Utawala mpya wa kijeshi nchini Niger umejitenga na washirika wake wa jadi wa mataifa ya Magharibi hasa Ufaransa, na umekuwa na mahusiano ya karibu na majirani zake wawili, ambao ni  Mali na Burkina Faso, ambazo pia kwa sasa zinaongozwa na wanajeshi baada ya mapinduzi.  

Soma pia: Mahakama ya ECOWAS yaamuru rais aliyepinduliwa Niger kuachiwa

Wanajeshi wa mwisho wa Ufaransa waliondoka Niger mnamo Desemba mwaka 2023. Kama ilivyo kwa nchi jirani za Burkina Faso na Mali, Niger inakabiliwa pia na uasi wa makundi ya kigaidi hasa katika eneo ambalo nchi hizo tatu za Sahel zinapakana.

Mwezi uliopita, rais wa Benin Patrice Talon alitoa wito wa kuanzishwa upya na kwa haraka uhusiano kati ya nchi yake na nchi jirani ya Niger. Wiki moja baadaye Benin iliondoa vikwazo kwa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje zinazopitia Niger kupitia bandari ya Cotonou baada ya miezi mitano ya vikwazo.

Kwa sasa uanachama wa Niger bado umesimamishwa katika  Jumuiya ya ECOWAS,  ambayo imesema kuachiliwa kwa Bazoum na kurejea kwake madarakani ni miongoni mwa masharti ya kulegezewa vikwazo.

Maafisa kadhaa wa serikali iliyopinduliwa wamekamatwa na wengine wamelazimika kwenda uhamishoni. Aliyekuwa waziri wa nishati Ibrahim Yacoubou alikamatwa wiki iliyopita aliporejea nchini humo.

(Chanzo: AFPE)