1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa mkulima atangazwa mshindi wa urais Peru

Sylvia Mwehozi
20 Julai 2021

Mwansiasa Msosholisti na mwalimu wa zamani wa shule Pedro Castillo amethibitishwa kushinda uchaguzi wa rais wa Peru, wiki sita baada ya matokeo rasmi kucheleweshwa kutokana na kuwepo na madai ya udanganyifu.

https://p.dw.com/p/3xkVj
Lima I Wahlen in Peru
Picha: Mariana Bazo/ZUMA/picture alliance

Mamlaka ya uchaguzi ya Peru imemtangaza Pedro Castillo kuwa rais ajaye, baada ya kushinda rasmi uchaguzi uliofanyika Juni 6 dhidi ya mpinzani wake Keiko Fujimori mwenye siasa za mrengo wa kulia. Matokeo hayo ya uchaguzi yalikuwa yamecheleweshwa baada ya kupingwa mahakamani na Fujimori kwa madai ya kugubikwa na udanganyifu.

Siku ya Jumatatu Fujimori, alisema kwamba atayatambua matokeo rasmi kwasababu anaheshimu sheria na katiba, lakini akaongeza kuwa ameibiwa kura.

"Leo ninatangaza kwamba, nitatimiza wajibu wangu! wajibu wangu kwa waperu wote, kwa Mario Vargas Llosa, kwa jumuiya ya kimataifa, kwamba nitatambua matokeo kwasababu sheria inasema hivyo na katiba niliyoapa kuitetea."

Keiko Fujimori mwanasiasa aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais Peru
Keiko Fujimori mwanasiasa aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais PeruPicha: Sebastian Castaneda/REUTERS

Waangalizi kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Canada na Uingereza walidai kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki. Castillo mwenye umri wa miaka 51 ambaye alikuwa mwalimu wa shule na mtoto wa mkulima ameahidi kuifanyia marekebisho katiba na kuongeza kodi dhidi ya makampuni ya uchimbaji madini. Peru ni taifa la pili ulimwenguni katika uzalishaji wa shaba. Mara baada ya kutangazwa, Castillo ametoa wito wa mshikamano na kuboresha uchumi. .

"Wakati huu ninatoa wito wa mshikamano kwa Waperu wote. Ninatoa wito wa umoja wa kitaifa na kufungua milango ya uhuru na kuifunga miaka hii ya tofauti zetu zote na shida zake zote."

Mamia ya wafuasi wake waliokuwa wamepiga kambi nje ya makao makuu ya Baraza la kitaifa la uchaguzi walijawa na furaha kufuatia tangazo hilo. Fujimori, ni binti wa rais wa zamani anayetumikia kifungo gerezani Alberto Fujimori. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 46 sasa anakabiliwa na mashitaka ya ufisadi katika kashfa inayohusiana na kampuni kubwa ya ujenzi ya Brazil inayodaiwa kufadhili juhudi zake za kuwania urais mwaka 2011 na 2016. Chini ya sheria za Peru kama angeibuka mshindi wa urais, kesi dhidi yake ingeahirishwa hadi pale atakapomaliza muhula wake madarakani. Rais mpya ataapishwa Julai 28.

Castillo ameapa kuwafurusha wageni wasio na vibali hususan Wavenezuela ambao waliwasili makumi kwa maelfu tangu mwaka 2017. Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mkuu wa chama cha wafanyakazi hakuwa anajulikana hadi pale alipoongoza maandamano ya nchi nzima miaka minne iliyopita yaliyoilazimu serikali kukubali madai ya nyongeza ya mshahara.

Vyanzo: AFP/Reuters