1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto mwingine wa Karume ataka kuwa rais wa Zanzibar

Salma Said15 Juni 2020

Harakati za uchaguzi mkuu Tanzania na Zanzibar uliosubiriwa kwa hamu na wanasiasa na wapiga kura, umeanza rasmi baada chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza kutoa fomu za kugombania urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.

https://p.dw.com/p/3do5Q
Sansibar Ali Karume Präsidentschaftskandidat
Ali Karume (kulia) baada ya kuchukua fomu za uteuzi wa chama cha CCM kwa ajili ya kugombea nafasi ya rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu Oktoba 2020. Picha: Salma Said

Rais wa sasa Dk Ali Mohamed Shein anamaliza muda wake wa urais baada ya kuwatumikia wananachi wa Zanzibar kwa miaka kumi kwa mujibu wa katiba, lakini awamu yake ya pili mwaka 2015 ilianza kwa mvutano baada ya uchaguzi huo kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Baadae uchaguzi huo ulirudiwa lakini ukasusowa na Chama Cha Wananchi CUF na hivyo kushindwa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao kwa kiasi kikubwa ilipunguza joto la kisiasa Zanzibar.

Aliyekuwa wa kwanza kuchukuwa fomu Jumatatu ni mwanachama wa CCM, mhandisi Mbwana Bakari Juma na kufuatiwa na Balozi Ali Abeid Karume ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar. Wakati Injia Mbwana akiahidi kuudumisha na kuuenzi Muungano, Halikadhalika Balozi Karume alisisitiza hilo.

Ali Mohammed Shein Zanzibar
Rais wa anaemaliza uda wake Dk Ali Mohammed Shein.Picha: DW/M. Khelef

Tofauti na uchaguzi uliopita ambapo uchukuwaji wa fomu wagombea wanakwenda kuchukuwa kwa shangwe kubwa, safari hii wagombea wamekwenda kuchukuwa fomu kimya kimya bila kusindikizwa na washangiliaji.

Mbali na amani, utulivu na upendo alivyoahidi kuvipa kipaumbele iwapo atapewa ridhaa na chama chake Karume pia aligusia kipaumbele kwa wanawake na watoto na kuendeleza yote yaliyotangulizwa na wenzake ambayo tayari yamo katika sera za chama cha Mapinduzi.

Uchukuwaji wa fomu umeanza Jumatatu na zoezi hilo litaendelea hadi Juni 30 na kufuatiwa na vikao vya CCM kupitisha jina moja la mgombea atakayemrithi Dk Shein akishinda urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Vyama vyengine vya upinzani vya ACT-Wazalendo ambacho mwenyekiti wake ni mwanasiasa Mkongwe, Maalim Seif Sharif Hamad, Chadema, CUF, na vyama vyengine pia wameanza harakati wa kutafuta wagombea wao.