1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtafaruku wa kisiasa Malaysia, Mahathir ajiuzulu

Sekione Kitojo
24 Februari 2020

Waziri mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammed amejiuzulu katika hatua ya kushangaza baada ya washirika wake kisiasa kutaka  kuiangusha serikali yake na kuzuwia kuingia madarakani kwa Anwar Ibrahim.

https://p.dw.com/p/3YKJW
Archivbild | Malaysia Putrajaya | Ministerpräsident Mahathir reicht seinen Rücktritt ein
Picha: Imago Images/H. Berbar

Hali hii  imekuja  baada  ya  miezi  kadhaa  ya kupanda  kwa  hali  ya wasi  wasi  katika  kile  kinachofahmika  kama " muungano  wa matumaini", ambao  uliingia madarakani  kwa  kushangaza mwaka 2018 dhidi  ya  serikali  iliyokuwa  imetumbukia  katika  rushwa ambayo  iliiongoza  Malaylasia kwa  miongo  sita.

Bildkombo- Mahathir Mohamad und Anwar Ibrahim
Mahathir Mohammed (kushoto) na Anwar Ibrahim (kulia)

Lakini  kulikuwa  na  miito kwa  Mahathir , kiongozi  mkongwe  kabisa duniani  mwenye  umri  wa  miaka  94, kuendelea  kubakia madarakani  kutoka  kwa  washirika  ambao  wanasisitiza  kuwa hakuunga  mkono  kuundwa  kwa  serikali  mpya  na  ameondoka kwa kukasirishwa  na  njama  hizo.

Patashika  hiyo  ya  kisiasa  ilianza  siku  ya  Jumapili wakati mahasimu  wa  Anwar  walipowasili  kutoka  muungano  unaotawala na  upinzani  walipofanya  vikao  kadhaa  mjini  Luala Lumpur, na kuzusha  uvumi  kuwa  ushirika  mpya  unaundwa.

Muungano huo  unaripotiwa  kuwa  ungemtenga  Anwar, mrithi mteule wa  Mahathir na  kiongozi  mkuu  wa  zamani  wa  upinzani  ambaye alifungwa  jela  kutokana  na  madai  yenye  shaka  ya  kulawiti, na kuzuwia  kuingia  kwake  madarakani  kuwa  waziri  mkuu.

Wakati  hatima  ya  serikali  bado  haifahamiki  hadi  leo  Jumatatu, Mahathir  aliwasilisha  barua  ya  kujiuzulu  kwa  mfalme. Mfalme amekubali  kujiuzulu  kwa  Mahathir, lakini  amemteua  kuwa  kiongozi wa  mpito  hadi  waziri  mkuu  mpya  atakapopatikana, kwa  mujibu wa  taarifa  rasmi.

Malaysia - Der malaysische König und Sultan von Kelantan Muhammad V heiratet.
Mfalme wa Malaysia Kelantan Muhammad VPicha: picture alliance/AP/V. Thian

Waziri mkuu  atoa  uhakika

Anwar, ambaye  amekuwa  na  uhusiano  usio mzuri  na  Mahathir, amesema  waziri  mkuu  amemhakikishia , kwamba  hakuhusika kabisa, na  juhudi za  kuunda  serikali  mpya, na  alikuwa  wazi kabisa  kuwa  hawezi kabisa  kufanyakazi  na  wale  ambao wanajihusisha  na  utawala  wa  zamani".

Muungano  mpya  unaopendekezwa  unaripotiwa  kuwa  unajumuisha chama  cha  United Malays National Organisation, UMNO, cha kiongozi  wa  zamani  Najib Razak, ambacho kiondolewa  madarakani miaka  miwili  iliyopita.

Anwar  na  Mahathir  waliweka  kando  tofauti  zao  na  kuweka nguvu  zao  pamoja na  kupambana  na  serikali  hiyo  iliyoingiliwa  na ugonjwa  wa  rushwa  katika  uchaguzi  wa  mwaka  2018. Mahathir , ambaye  aliwahi  kuwa  waziri  mkuu  kuanzia  mwaka  1981  hadi 2003, alitoa  ahadi  ya   kabla  ya  uchaguzi  ya  kukabidhi  madaraka kwa  Anwar  lakini  mara  kwa  mara  alikuwa  anakataa  kuweka tarehe  ya  makabidhiano.

Anwar Ibrahim
Anwar IbrahimPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Thian

Muda  mfupi  kabla  ya  kujiuzulu , chama  cha  Mahathir  cha Bersatu  kilijitoa  kutoka  katika  muungano  unaounda  serikali  na wabunge  kadhaa  walijiuzulu  kutoka  katika  chama  cha  Anwar, wakauacha muungano wa   makubaliano  ya  matumaini katika  hali mbaya  na  kuchochea fununu  kuwa  juhudi  ziko  mbioni  kuunda ushirika  mpya. Mahathir  pia  amejiuzulu  kuwa  mwenyekiti  wa chama  chake  cha  Bersatu.