1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msukosuko unaowakuba wakimbizi kutoka Afrika

24 Desemba 2004

Watu kumi na tatu wenye asili ya Kiafrika waliokuwa wakijaribu kuingia nchini Uhispania kupitia njia za mkato,walipoteza maisha yao baada ya kupigwa na baridi kali na boti lao kuzama katika bahari ya Uhispania.

https://p.dw.com/p/CEHE
Mpaka wa senyen'ge baina ya Uhispania na Moroko
Mpaka wa senyen'ge baina ya Uhispania na MorokoPicha: AP

Tukio hilo limedhihirisha wazi jinsi waafrika wanavyopania kuingia katika mataifa ya Ulaya bila kujali hatari zilizopo katika njia wanazotumia kuingia Ulaya. Kwa mujibu wa maafisa wa polisi wa Uhispania watu hao kumi na tatu walipatikana wakiwa tayari wameshafariki siku ya Alhamisi baada ya kuvamiwa na baridi kali walipokuwa wakisafiri kwa boti lao kuelekea visiwa vya canary vilivyo ndani ya Uhisania. Polisi wamesema baada ya kuona boti hilo katika kisiwa cha Fuerteventura mojawapo ya visiwa hivyo vya Uhispania, walituma boti lao mara moja kulivuta boti hilo hadi ufuoni.

Kulingana na taarifa kutoka Uhispania, baadhi ya wengine waliokolewa walipatikana ndani ya boti hilo,wakiwa wamelalia maiti za wenzao pengine kujizuia na baridi.

Watu thelathini waliokolewa ,lakini watatu kati yao walikuwa katika hali mahututi na ilibidi kupelekwa hospitali mara moja.

Wahamiaji hao waliokuwa wamevalia mavazi mepesi kabisa wanasemekana kusafiri kwa muda wa siku tatu mfululizo katika bahari hiyo, huku wakivumilia baridi kali na mvua, ijapokuwa haikutambulika mara moja walitokea upande gani.

Cha ajabu zaidi na vilevile cha kusikitisha ni kwamba katika safari yao hiyo hawakuwa na mafuta,maji wala chakula chakuwawezesha kuishi kwa muda wa siku tatu hizo.

Afisa wa usalama katika kisiwa hicho cha Fuerteventuran,alithibisha kwamba watu hao kumi na tatu walifariki kutokana na baridi kali iliyowaingia mwilini, aliendelea kusema kuwa haisaidii lolote kwa wahamiaji kutumia njia za mkato tena hatari,kwani bahari hiyo ni mbaya na pindi watu wanapolowama maji basi huwa ni hatari zaidi.

Hapo jumatano pia wengine wawili walifariki wakijaribu kuingia Uhispania lakini wenzao 35 waliokolewa baada ya boti lao kukabiliwa na mawimbi makali katika visiwa hivyo vya canary.

Visa kama hivi vinatokea kila mwaka,ambapo maelfu ya waafrika wanajaribu kukimbilia mataifa ya ulaya kutafuta maisha mazuri,kupitia njia hatari na za kuogofya mno.

Kundi moja linaloshughulikia wahamiaji kutoka Morocco linalojiita ATIME limekisia idadi ya watu 4000 wameshafariki tangu mwaka 1997 kupitia njia kama hii. Kwa mujibu wa serikali ya Uhispania kuanzia katikati ya mwezi Septemba mwaka huu zaidi ya watu 10,000 wamekamatwa na kutiwa ndani kutokana na kosa la kuingia nchini humo kinyume cha sheria. Nusu ya idadi hiyo ni wahamiaji kutoka Morocco,na idadi kubwa kutoka nchini Mali na Gambia.

Mawaziri kutoka Ulaya na Afrika ya Kaskazini mwezi uliopita walijadili pendekezo la kusaidia kuimarisha maisha ya wakazi wa Afrika ili kuzuia hatari kama hizi kutokea.

Lakini pendekezo la Ujerumani la kuundwa kwa kambi za wakimbizi ndani ya Afrika ya Kaskazini ili kuwazuia kuingia ulaya kupitia bahari ya Mediterranean limeonekana kupuuzwa kwa sasa. Limezua hisia kwa mataifa mengi wanachama wa umoja wa Ulaya kuhusu gharama na haki za binadamu.

Jitihada zinaendelea kufanywa na mataifa 25 wanachama wa umoja wa Ulaya kuzuia ongezeko la wahamiaji kinyume cha sheria,ambao huatarisha maisha yao kila siku kuingia Ulaya hasa kutoka Afrika ya Kaskazini.

Kufikia sasa sheria zimeongezeka katika mataifa ya Ulaya na nchi nyingi zinashinikizwa kuzuia wahamiaji kinyume cha sheria na kupunguza idadi ya wanaomba kibali cha kuwa wakimbizi.