1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Mshukiwa wa mauaji ya Monterey Park ajiuwa

23 Januari 2023

Polisi ya Marekani imesitisha juhudi za kumtafuta mtu aliyejihami kwa bunduki na kuwauwa watu 10 huko California, katika sherehe za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Lunar baada ya kuupata mwili wake ukiwa katika gari.

https://p.dw.com/p/4MZEJ
USA | Polizeieinsatz in Monterey Park
Picha: Frederic J. Brown/AFP/Getty Images

Mkuu wa polisi wa Los Angeles Robert Luna amesema wameupata mwili huo ukiwa na jeraha la risasi aliyojifyatulia mwenyewe.

"Mshukiwa ametambuliwa kama Huu Can Tran. Ni mwanamume aliye na umri wa miaka 72 na mwenye asilia ya Asia. Ninathibitisha kwamba hakuna washukiwa wengine kutokana na tukio hilo la mauaji katika uwanja wa Monterey," alisema Luna.

Luna ambaye katika mkutano na waandishi wa habari, hakuweza kutaja umri kamili wa wahanga wa tukio hilo, amesema wote walionekana kuzidi umri wa miaka 50. Kulingana na Luna, saba kati ya watu kumi waliojeruhiwa bado wako hospitali.

Mwili ulikuwa na jeraha la risasi

Inaarifiwa kwamba baada ya kufanya mauaji hayo katika eneo la kwanza, dakika chache baadae mtu huyo alijaribu kwenda katika klabu nyengine na kuanza tena kufyatua risasi ila mamlaka zinasema, watu wawili walipambana naye na kumpokonya silaha aliyokuwa nayo kabla hajaanza ufyatuaji, ndipo alipotoweka.

USA | Polizeieinsatz in Monterey Park
Mmoja wa waliojeruhiwa akiingizwa kwenye gariPicha: TNLA/Handout/REUTERS

Polisi waliupata mwili wa Tran ukiwa unaning'inia katika sehemu ya gurudumu ya gari alilokuwa amelitumia kukimbia ukiwa na jeraha la risasi. Gari hilo lilipatikana katika eneo la Torrance, ambalo ni eneo jengine lenye idadi kubwa ya Wamarekani wenye asili ya Asia.

Maafisa wanaochunguza tukio hilo bado hawajafahamu sababu ila matukio ya ufyatuaji wa risasi hutokea mara kwa mara nchini Marekani.

Tukio hilo lililofanyika katika mji wa Moterey Park ambalo ni eneo lenye idadi kubwa ya Wamarekani wenye asili ya Asia, lilitilia kiwingu sherehe hizo ambazo kwa kawaida zinaadhimishwa China, Vietnam na Korea Kusini na kuitia hofu jamii hiyo ya Wamarekani wenye mizizi ya Asia.

Mauaji ni ya tano makubwa kufanyika mwezi huu

Sherehe hizo za Monterey Park ni mojawapo ya sherehe kubwa zaidi za Mwaka Mpya wa Lunar huko California. Kulikuwa kumeratibiwa kufanyika sherehe za siku mbili ila maafisa walifutilia mbali sherehe za jana kufuatia mauaji hayo yaliyotokea.

USA, | Polizeieinsatz in Monterey Park
Polisi wakipiga doria Monterey ParkPicha: Frederic J. Brown/AFP/Getty Images

Mauaji hayo ni ya tano makubwa kufanyika nchini Marekani mwezi huu. Aidha ndiyo mauaji mabaya zaidi kufanyika tangu Mei 24 mwaka jana ambapo watu 21 waliuwawa katika shule moja huko Uvalde jimboni Texas.

Rais Joe Biden na Mkuu wa Sheria Merrick Garland waliambiwa kuhusiana na tukio hilo na wameziagiza mamlaka za shirikisho kusaidia katika uchunguzi wa tukio hilo.

Chanzo: AP/Reuters