1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshirika wa Trump alikiuka vikwazo vya kuingiza silaha Libya

Yusra Buwayhid
20 Februari 2021

Ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa inadai kwamba Prince alimsaidia mbabe wa kivita wa Libya Khalifa Haftar kwa kumpatia silaha na mamluki wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/3pdQQ
Erik Prince Blackwater
Picha: Imago/UPI Photo

Mkandarasi binafsi wa masuala ya usalama na mshirika la rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, Erik Prince, anatajwa kukiuka marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya ya Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, ambayo pia nakala yake imeonekana na vyombo vya habari vya Marekani.

Kulingana na ripoti hiyo ya siri ya Baraza la Usalama, iliyoonekana na magazeti ya New York Times na Washington Post, Prince alipeleka kikosi cha wapiganaji mamluki na silaha kwa mbabe wa kivita Khalifa Haftar, ambae 2019 alikuwa akipigana kuiondoa madarakani serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Operesheni hiyo ya dola milioni 80 ilijumuisha mipango ya kuunda kikosi kitakachowafuatilia na kuwaua makamanda wa Libya wanaompinga Haftar, pamoja na wadau wengine ambao walikuwa raia wa mataifa ya Umoja wa Ulaya, limesema gazeti la New York Times.

Kulingana na jopo la wataalamu katika Umoja wa Mataifa, Erik Prince akiwa mjini Cairo mwaka 2019 alipendekeza operesheni ya kijeshi ya kumsaidia Haftar kupambana na serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kama sehemu ya kile kilichoitwa "Operesheni Opus", Prince alipendekeza kumsaidia Haftar kwa ndege na meli za kivita pamoja na kushirikiana nae katika kuandaa mpango wa kuwateka nyara mahasimu wake wa ngazi za juu.

Ripoti hiyo inasema kufuatia makubaliano hayo, Prince alituma ndege za kivita nchini Libya na kuikiuka marufuku ya Umoja wa Mataifa ya kuingiza silaha nchini humo.

Prince, mwanajeshi wa zamani wa kikosi cha majini cha Marekani na ndugu wa aliyekuwa waziri wa elimu Betsy DeVos, amekuwa mshirika wa karibu wa Trump katika miaka ya hivi karibuni.

Prince anaweza kuwekewa vikwazo

Operesheni hiyo iliwahi kuripotiwa na shirika la habari la dpa mnamo mwezi Mei, likinukuu wataamu wa Umoja wa Mataifa, lakini bila ya taarifa zozote zinazomhusisha Prince na kadhia hiyo.

Gazeti la New York Times limesema kwa tuhuma hizo, upo uwezekano wa Umoja wa Mataifa kumwekea Prince vikwazo, vikiwemo vya marufuku ya kusafiri nje ya Marekani.

Ägypten Präsident  al-Sisi (R) trifft Rebellen-Führer Haftar aus Libyen
Rais wa Misri al-Sissi (kulia) na Jenerali Khalifa Haftar (kushoto)Picha: picture-alliance/AA/Presidency of Egypt

Prince alikataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa, na mwanasheria wake amekataa kutoa tamko lolote juu ya kadhia hiyo, limeongeza gazeti la New York Times.

Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta imetumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kulipozuka vuguvugu la maandamano liloungwa mkono na NATO na kumuondoa madarakani Muammar Kadhafi mwaka 2011.

Katika miaka ya hivi karibuni, taifa hilo limegawanyika kati ya Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa (GNA) mjini Tripoli, na utawala wa mashariki mwa nchi unaoongozwa na mbabe wa kivita Haftar, anaekabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita.

Mnamo mwaka 2019, wakati Trump akiwa rais wa Marekani, alimsifu mbabe huyo wa kivita kwa mchango wake wa " kupambana na ugaidi" nchini Libya.

Serikali mpya ya mpito iliyochaguliwa mnamo Februari 5 na Kongamano la Majadiliano ya Kisiasa la Libya huko Uswizi, inajumuisha washiriki 75 waliochaguliwa na Umoja wa Mtaifa kuwakilisha sehemu pana ya jamii nchini humo. Na Haftar ameunga mkono uteuzi huo.

Vyanzo: afp,dpa