1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wawasili kwa wingi kwa wahanga wa tetemeko Haiti

20 Agosti 2021

Msaada umeanza kuwasili kwa wingi kwa wahanga wa janga la Tetemeko la Ardhi lililoikumba Haiti lakini hali duni ya miundombinu nchini humo bado inatatiza zoezi hilo kuwafikia watu wengi waliathirika. 

https://p.dw.com/p/3zCH4
Haiti | Tropensturm Grace nach Erdbeben
Picha: Henry Romero/REUTERS

Misaada kutoka kwa taasisi binafsi na shehena nyingine iliyotumwa na Marekani na mataifa mengine imeanza kulifikia eneo la kusini magharibi mwa Haiti ambako tetemeko kubwa la ardhi la Jumamosi iliyopita limewauwa zaidi ya watu 2,100

Marekani ambayo imekuwa ikituma msaada nchini Haiti tangu kutokea kwa Tetemeko, siku ya Alhamisi ilituma  helikopta 10 za jeshi kupeleka vikosi vya uokozi, wafanyakazi wa huduma za afya na mahitaji muhimu nchini humo.

Meli ya jeshi la Marekani USS Arlington inatarajiwa pia kuwasili mwishoni mwa juma ikiwa na shehena ya msaada unaohitajika.

Mkuu wa kamandi ya jeshi la Marekani anayesimamia operesheni za kuisaidia Haiti Craig Faller amesema serikali mjini Washington inaendelea kufanya kazi na mamlaka za Haiti kubaini kiwango cha madhara yaliyotokea na wale waliopoteza maisha au kujeruhiwa.

Mataifa mengine ikiwemo Ujerumani pia yametuma timu za uokoaji na msaada wa matibabu kwenda Haiti.

Hasira na fadhaa kutokana na msaada kuwasambazwa kwa mwendo wa kobe 

Hata hivyo kusuasua kwa usambazaji wa misaada kumezidisha hasira na fadhaa kwa wahanga ambao wengi wamepoteza nyumba, hawana sehemu salama za kulala na wanabangaiza kupata vyakula

Haiti | Tropensturm Grace nach Erdbeben
Wengi ya wahanga bado wanasubiri msaada nchini HaitiPicha: Henry Romero/REUTERS

Taarifa zinasema juhudi za kusambaza mahitaji zinakwenda kwa mwendo wa kobe kutokana na athari ya mvua kubwa iliyonyesha katikati ya wiki baada ya janga lingine la asili la kimbunga kilichopewa jina Grace kukipiga kisiwa hicho cha Karrebian.

Katika uwanja mdogo wa ndege kwenye mji wa Les Cayes, miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi, polisi ililazimika kufyetua risasi kuwatawanyawa watu walioangusha wigo wa sinyenge kuyavamia malori yaliyobeban msaada.

Mkaazi mmoja wa eneo hilo Filina Merzy ambaye amepoteza karibu kila kitu  amesema "Wakati mwingine hukaa hapa na kulia, nikitizama jinsi nilivyopoteza kila kitu. Sina chochote. Pengine Mwenyezi Mungu atatuma mtu kunisaidia. Nimesalia na Mungu pekee. Siku nyingine sina chakula, jirani akipika ndiyo hunipatia sahani ya chakula. Maisha na mazingira kwenye uwanja huu wa mpira siyo rahiis, Ninajihisi mgonjwa na ningependa kupata msaada na nyumba ya kuishi."

Utekaji nyara wa madaktari wazidisha kishindo 

Haiti | Tropensturm Grace nach Erdbeben
Kambi za muda nchini Haiti Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Hadi kufikia leo Ijumaa shirika la Usalama wa Umma nchini Haiti limesema idadi ya waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi imepanda na kufikia watu 2,189 na wengine 12,268 wamejeruhiwa.

Taarifa pia zinasema watu wengine wasiopungua 300 bado hawajulikani waliko tangu tetemeko la ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha Richter lilipokipiga kisiwa hicho na kufanya uharibu wa majengo na miundombinu.

Inaarifiwa hali imekuwa mbaya zaidi kwa waliojeruhiwa na Tetemeko la Ardhi baada ya hospitali kuu kwenye mji mkuu Port-au-Prince kutangaza kufunga shughuli zake kwa siku mbili kulaani kutekwa nyara kwa madaktari bingwa wawili kulikofanywa na magenge ya wahalifu.

Miongoni mwa mwa waliotekwa ni daktari bingwa upasuaji nchini humo na kisa hicho kimeongeza chumvi kwenye kidonda katika wakati serikali inayaribu kuyathibiti makundi ya wahalifu yanayotishia kutatiza usambazaji misaada ya dharura.

Mwandishi: Rashid/AP/DPA