1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa biashara yumkini ukapunguza fedha katika afya na elimu Afrika.

Mohamed Dahman22 Julai 2007

Serikali za Afrika zina wasi wasi kwamba michango ya fedha kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuzisaidia kuongeza fungu la nchi zao la biashara duniani itatumika kama aina nyengine ya msaada wa maendeleo.

https://p.dw.com/p/CHk3
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akisalimiana na Waziri Mkuu wa Danmark Anders Fogh Rasmussen wakati wa Kikao cha Ushirikiano na Afrika kilichofanyika Berlin Ujerumani mwezi wa Mei mwaka 2007.Katikati ni Rais wa Bhotswana Festus Mogae.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akisalimiana na Waziri Mkuu wa Danmark Anders Fogh Rasmussen wakati wa Kikao cha Ushirikiano na Afrika kilichofanyika Berlin Ujerumani mwezi wa Mei mwaka 2007.Katikati ni Rais wa Bhotswana Festus Mogae.Picha: AP

Nchi hizo za Kiafrika zinaona msaada huo kwa ajili ya biashara unaweza kupunguza michango ya fedha kwa ajili ya sekta za afya na elimu barani humo.

Chombo kikuu cha utendaji katika Umoja wa Ulaya yaani Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imekuwa ikitowa ahadi kwamba msaada mkubwa kwa ajili biashara utapatikana kwa ajili ya nchi za za Afrika,Carribean na Pasifiki ACP ambazo zinajiandaa kusaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Umoja wa Ulaya EPA ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Msaada huo unakusudia kushughulikia tatizo la uwezo mdogo wa biashara wa nchi za ACP suala muhimu likiwa kwa nini nchi za kimaskini duniani hufanya biashara pungufu ya asilimia moja katika kusafirisha nje bidhaa zao duniani.Fedha hizo pia zitasaidia nchi za ACP kutimiza viwango vya usalama wa wanyama na chakula vya Umoja wa Ulaya.

Hapo mwezi wa Mei serikali za Umoja wa Ulaya na Halmashauri ya umoja huo zimejifunga kutowa ruzuku ya euro bilioni mbili katika msaada wa kila mwaka kwa biashara ifikapo mwaka 2010.

Juu ya kwamba maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema kwamba nchi za ACP zitapatiwa kima hicho kikubwa cha fedha baadhi ya wanadiplomasia wa nchi za Kiafrika hawakuridhishwa na hilo.Wanadai kwamba asasi kubwa kabisa za Umoja wa Ulaya bado hazikufafanuwa hasa fedha hizo zitatoka wapi au kuondowa wasi wasi kwamba hazitokuwa ziada ya msaada ambao ungeliweza kutumiwa kwa ajili tu ya kugharamia uwekezaji unaohitajika katika sekta ya afya na elimu.

Mwanadiplomasia mmoja wa Afrika akizungumza bila ya kutaka kutajwa jina amesema kwamba Umoja wa Ulaya tatizo la msaada kwa biashara ni kwamba kwa kiasi kikubwa sana haufafanuliwi.Anasema Umoja wa Ulaya unatumia ahadi zake za msaada kwa ajili ya biashara kuzishawishi nchi za ACP kusaini makubaliano ya EPA licha ya wasi wasi kwamba kiwango cha ufunguzi wa masoko kinachohitajika kama sehemu ya makubaliano hayo kitayawacha mashirika ya kienyeji hatarini kutokana na ushindani kutoka nje.

Kwa mujibu wa Katrin Jansen msaidizi wa mipango na shirika la Wanawake katika Maendeleo Barani Ulaya lenye makao yake mjini Brussels Ubelgiji msaada kwa ajili ya biashara moja kwa moja utakuwa badala ya aina nyengine ya msaada wa maendeleo.

Anasema wana wasi wasi sana juu ya jambo hilo na wanadai msaada kwa ajili ya biashara usiondolewe kutoka sekta kama vile elimu na afya kwa sababu sekta hizo kimsingi zinaendelea kuwa muhimu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kadhalika kwa ajii ya maisha katika nchi zinazoendelea.

Umoja wa Ulaya umekuwa hauko tayari kutowa msaada zaidi kwa ajili ya biashara kwani kufanya hivyo kutahusisha kukiri kwamba changamoto inazorithi Makubaliano ya Ushirikiano wa Biashara kati ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya EPA ni kubwa kwa nchi za kimaskini kuliko vile ilivyokuwa imejiandaa kukiri hadi sasa na hiyo kupunguza uwezekano kwamba makubaliano hayo yatakamilishwa tarehe 31 Desemba siku ya mwisho iliotajwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Afisa wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya maendeleo amekanusha kwamba halmashauri hiyo inataka kuzitumia upya fedha walizoahidi awali.Ameeleza kwamba nakala ya karibuni ya Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya itaanza tu kufanya kazi hapo mwezi wa Januari mwaka 2008 wakati msaada kwa ajili ya fedha za biashara unaweza kuanza kusambazwa kabla ya hapo.