1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa ugonjwa kama Ebola wasababisha vifo DRC

John Kanyunyu30 Julai 2018

Watu kumi na watano wameripotiwa kupoteza maisha kufuatia ugonjwa wa kuharisha, kutapika na kutokwa damu mwilini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

https://p.dw.com/p/32Ir3
DR Kongo Ebola Ausbruch
Picha: Reuters/K. Katombe

Kumeripuka ugonjwa wa kuharisha, kutapika na kutokwa damu mwilini katika wilaya ya Beni, mji wa Beni na pia wilaya ya Mambasa katika mkoa wa Ituri.

Watu kumi na watano wameripotiwa kupoteza maisha kufuatia ugonjwa huo katika mji mdogo wa Mangina, kilomita thelathini magharibi mwa mji wa Beni.

Akizungumza na wanahabari kuhusu kuripuka kwa ugonjwa huo katika mji mdogo wa Mangina, naibu Meya wa mji wa Beni Bakwanamaha Modeste, aliwahimiza wakazi wa mji wake kuheshimu taratibu za usafi, ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ambao bado haujajulikana.

Ugonjwa huo ulizuka siku chache tu baada ya serikali ya DRC kutangaza mwisho wa ugonjwa wa Ebola
Ugonjwa huo ulizuka siku chache tu baada ya serikali ya DRC kutangaza mwisho wa ugonjwa wa EbolaPicha: Reuters/K. Katombe

Ugonjwa huo ukiwa unaambukizwa kwa kupitia kumgusa mgonjwa na kwa njia nyinginezo, kuripuka kwake katika mji mdogo wa Mangina, pamoja na mji wa Beni, kumezusha wasiwasi miongoni mwa wakazi wa mji wa Beni, ambako ugonjwa huo usiojulikana hadi sasa umeripotiwa kuwaathiri watu watatu. Hayo yameelezwa na afisa wa afya mjini Beni, daktari Michel Tosalisana.

Kwa mujibu wa ripoti katika radio ya RTR, mjini Beni, watu kumi na watano wamefariki dunia kufuatia ugonjwa huo katika mji mdogo wa Mangina. Watatu kati ya wagonjwa watano walioambukizwa ugonjwa huo wamefariki dunia katika mkoa wa Ituri, eneo linalopakana na mji mdogo wa Mangina, katika mkoa wa Kivu kaskazini.

Ugonjwa huo uliozuka siku chache tu baada ya serikali ya DRC kutangaza mwisho wa ugonjwa wa Ebola katika nchi hii, unadhaniwa na wengi kuwa huenda serikali ikatangaza upya mripuko wa ugonjwa wa Ebola, ikiwa sampuli zilizopelekwa kwenye mahabara maalumu, zitaonesha kuwa ni virusi vya Ebola vinavyowaangamiza wakazi katika mji mdogo wa Mangina, na ambao kumeripotiwa pia katika mji huu wa Beni.

Watu 15 wameripotiwa kufariki dunia kufuatia ugonjwa huo katika mji mdogo wa Mangina
Watu 15 wameripotiwa kufariki dunia kufuatia ugonjwa huo katika mji mdogo wa ManginaPicha: Reuters/K. Katombe

Tatizo kubwa katika eneo hili ni kuwa, watu wanao uzoefu wa kula nyama za pori, bila ya kujuwa ikiwa nyama hizo zinazouzwa mitaani ni za wanyama waliouawa na wawindaji, au walifariki porini kwa magonjwa.

Kupigwa marufuku uwindaji, uuzaji na ulaji wa nyama toka mbuga za wanyama na taasisi inayohusika na kuhifadhi wanyama wa porini ICCN, kunaonekana kutoheshimiwa na wakazi, wanaowinda, kuuza na kula nyama za pori.

Na kabla ya matokeo ya mahabara kutangazwa, kaimu Mea wa mji wa Beni Bakwanamaha Modeste, ametoa mwito huu kwa wakazi wa mji wake kutahadhari.

Vituo vyote vya afya katika mji wa Beni, vimeombwa na Meya wa mji, kuwaongoza wagonjwa walioambukizwa kwenye hospitali kuu ya Beni, ambako watahudumiwa ipasavyo.

Mwandishi: John Kanyunyu DW, Beni.

Mhariri: Yusuf Saumu