1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpinzani wa kisiasa akamatwa kwa madai ya ubakaji Rwanda

Saleh Mwanamilongo
10 Septemba 2021

Profesa wa Chuo Kikuu na mmoja wa viongozi wa upinzani nchini Rwanda Christopher Kayumba amekamatwa mjini Kigali. Polisi wanamtuhumu kwa makosa ya ubakaji.

https://p.dw.com/p/409sy
Ruanda | Paul Rusesabagina | Anklage erhoben
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kwa mujibu wa Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda (RIB) ni kwamba Christopher Kayumba anakabiliwa na madai yaliyowasilishwa na watu kadhaa, akiwemo mwanafunzi wake wa zamani.

Taarifa ya RIB imesema Mhadhiri huyo wa zamani wa chuo cha uandishi habari cha mjini Kigali, alikamatwa alhamisi baada ya kipindi cha kuchunguzwa kufuatia tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia zilizotolewa na watu kadhaa.

Christopher Kayumba, mwenye umri wa miaka 48, anaendesha gazeti la mtandaoni linaloitwa "The Chronicles" na alianzisha chama cha kisiasa cha upinzani dhidi ya Rais Paul Kagame mnamo mwezi Machi.

Muda mfupi tu baada ya kuanzisha chama hicho, Kayumba alikabiliwa na madai ya ubakaji, ambayo kwanza yaliibuka mitandaoni. Lakini alikanusha tuhuma hizo.

''Kila mwanasiasa anatishiwa''

Kukamatwa kwa Christopher Kayumba kumeibua hisia mseto nchini Rwanda. John Williams Ntwali, mwandishi habari na mchambuzi kutoka Rwanda amesema wengi wanadhani kwamba kukamatwa kwake kunatokana na sababu za kisiasa.

''Ni wachache sana wanaoamini kwamba Christopher Kayumba alifanya uhalifu huo,lakini walio wengi wamesema ni tuhuma zisizo na msingi wowote, na kwa sababu ni mwanasiasasa na kila mwanasiasa hapa anatishiwa na kufunguliwa mashtaka.'',alisema Ntwali.

Juhudi zetu za kuwapata maafisa wa ofisi ya upelelezi ya Rwanda (RIB) hazikufanikiwa.

Jela au kuhojiwa kwa wakosoaji wa serikali

Wakosoaji wengi wa  rais Kagame wako gerezani au wahojiwa na idara ya upepelezi
Wakosoaji wengi wa rais Kagame wako gerezani au wahojiwa na idara ya upepeleziPicha: Getty Images/A. Renneisen

Christopher Kayumba alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa "usumbufu wa umma" baada ya maafisa wa usalama wa uwanja wa ndege kukataa kumruhusu kusafiri kwenda Nairobi mnamo Desemba 2019. Mamlaka ilisema Kayumba alikuwa ametokea uwanja wa ndege akiwa amechelewa na alikuwa amelewa na alitishia kuufunga uwanja huo.

Mnamo Juni, profesa mwingine wa chuo kikuu, Aimable Karasira, ambaye alimkosoa Kagame kwenye mtandao wa Youtube, alishtakiwa kwa shutuma za kutoa kauli inayohalalisha mauwaji ya kimbari. Hadi sasa anashikiliwa mjini Kigali. Wakosoaji wengine wa serikali ya Rwanda, mfano wa Yvonne Idamange na Rashid Hakuzimana wamekamatwa au kuhojiwa na idara ya upelelezi ya Rwanda.

Kukamatwa kwa Christopher Kayumba kunatokea wiki moja baada ya kufariki akiwa kizuizini mwanamuziki maarufu wa miondoko ya Rap nchini Rwanda Joshua Tuyishime maarufu kama Jay Polly.

Polly ni mwanamuziki wa pili kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha nchini Rwanda katika muda usiopungua miaka miwili, baada ya Kizito Mihigo ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumande.