1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mparaganyiko mkutano wa COP25

Admin.WagnerD13 Desemba 2019

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP25 unaelekea kuhitimishwa mjini Madrid, Uhispania lakini matokeo yake hayatofikia malengo ya kukabiliana na kitisho cha ongezeko la joto duniani.

https://p.dw.com/p/3Ulzi
Spanien UN-Klimakonferenz 2019 COP 25 l Außenansicht Messe
Picha: Reuters/S. Vera

Mkutano wa COP25 umefanyika wakati ulimwengu ukishuhudia mfululizo wa majanga ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo vimbunga visivyotarajiwa, ukame na wimbi la joto kali.

Wanasayansi wamekusanya ushahidi wa kutosha kuonesha athari mbaya zaidi zitakazoukumba ulimwengu katika muda mfupi unaokuja huku mamilioni ya wanaharakati vijana wa mazingira wakiongoza maandamano ya kila wiki kudai hatua zaidi za serikali duniani kukabiliana na athari za uchafuzi mazingira.

Wakati shinikizo linaongezeka ndani na nje ya mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi, hoja zinazoleta migawanyiko kati ya mataifa tajiri yanayoongoza kwa utoaji wa gesi ukaa na yale masikini zimeibuka upya.

Zaidi ni kuhusu nani anapaswa kupunguza utoaji gesi ya ukaa na vipi matrilioni ya dola yatalipwa kusaidia maisha ya watu katika ulimwengu ulioharibiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Wajumbe wanajaribu kutafuta makubaliano

Spanien Madrid Greta Thunberg (C) und Luisa Neubauer (R)
Picha: Imago Images/Agencia EFE

Katika saa za lala salama wajumbe wa mazungumzo ya mjini Madrid wamekuwa wakijaribu kuvifanyia marekebisho vipengele kadhaa wakilenga kufikia makubaliano yanayoeleweka kuhusu biashara ya gesi ya ukaa na msaada kwa mataifa masikini yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo wafuatiliaji wa COP25 wamesema wajumbe wa majadiliano mjini Madrid wameshindwa kutimiza malengo ya kauli mbiu ya mkutano huo iliyohimiza kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua.

Hata uwepo wa mwanaharakati kijana wa mazingira, Greta Thunberg haukusaidia chochote katika kuongeza ahadi za mataifa duniani za kupunguza utoaji wa gesi ya ukaa.

Mataifa yanayoendelea yameitaja Marekani kuwa moja ya nchi zinazokwamisha mazungumzo kuhusu msaada unaopaswa kutolewa kwa nchi masikini ulioridhiwa mwaka 2013.

Maafisa wa Marekani wameyatupilia mbali madai hayo.

Mkataba wa Paris utafanikiwa?

Madrid Cop25
Picha: Reuters/S. Vera

Kwa sehemu fulani, lengo la mkutano wa Madrid lilikuwa ni kukamilisha kanuni za utekelezaji mkataba wa Paris wa mwaka 2015 ambao unayataka mataifa kuzuia kiwango cha joto duniani kupindukia nyuzi 1.5 katika kipimo cha Celsius.

Dunia tayari imefikia kiwango cha nyuzijoto 1 na kinaelekea kupanda hadi nyuzi mbili au tatu ifikapo mwaka 2100 lakini mataifa ulimwenguni bado yanapuuza umuhimu wa kupunguza viwango vya uchafuzi hata wakati wa mkutano wa Madrid.

Muda wa mwisho uliowekwa na mkataba wa Paris kwa mataifa kutoa ahadi za kupunguza viwango vya uchafuzi ni 2020.

Mkutano wa Madrid ulilenga kuwa uwanja kwa mataifa duniani kuonesha nia madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi.

Lakini ni mataifa 80 pekee yanayowakilisha asilimia 10 ya viwango vya utoaji gesi ukaa ndiyo yameahidi kufanya zaidi kupunguza viwango vya uchafuzi.