1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yakata ushirikiano na ubalozi, taasisi za Kijerumani

2 Machi 2021

Morocco imetangaza kuacha mashirikiano na mawasiliano yoyote na ubalozi wa Ujerumani kutokana na msimamo wa serikali ya Ujerumani kuelekea Sahara ya Magharibi na pia kutohusishwa mkutano wa amani ya Libya.

https://p.dw.com/p/3q5gQ
Markokko l König Mohammed VI empfängt Russischen Außenminister Lawrow in Rabat
Picha: picture alliance/dpa/TASS/A. Sherbak

Waraka uliotolewa leo (Machi 2) na wizara ya mambo ya kigeni ya Morocco na kushuhudiwa na shirika la habari la Reuters, unaelezea suintafahamu kubwa kabisa kama sababu ya kuzitaka wizara na vyombo vya serikali kujiepusha na mawasiliano yoyote na siyo tu ubalozi, bali hata mashirika ya misaada na taasisi za kisiasa za Ujerumani. 

Hata hivyo, waraka huo haukueleza undani wa "suintafahamu" hizo. Mwandiplomasia mmoja wa ngazi za juu alitaja hatua ya Ujerumani kwa uamuzi wa Marekani wa mwezi Disemba kuitambuwa Sahara Magharibi kama sehemu ya Morocco, na pia uamuzi wa Ujerumani wa kutokuialika Morocco kwenye mkutano wa kimataifa juu ya Libya uliofanyika mwaka jana. 

Baada ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kuyatambuwa mamlaka ya Morocco kwenye jimbo hilo la Sahara Magharibi, Ujerumani iliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili suala hilo.

Kwa miaka kadhaa sasa, Morocco imekuwa ikichukuwa dhima kubwa kwenye mahusiano ya kidiplomasia nchini Libya, ikiendesha vikao vya mazungumzo baina ya wajumbe mbalimbali wa makundi hasimu, kando ya vikao vilivyoratibiwa na Umoja wa Mataifa mjini Berlin mwaka jana.

Sahara Magharibi na Libya

Algerien | Smara Flüchtlingslager Sahrauis
Wakimbizi wa Sahara Magharibi kwenye kambi ya Smara.Picha: Louiza Ammi/abaca/picture alliance

Kwa Ujerumani kuujadili msimamo mpya wa Marekani kuhusu hadhi ya Sahara Magharibi na pia kutokuihusisha kwenye mkutano huo wa Berlin, hapana shaka ilitafsiriwa na Morocco kama ni dharau ya mamlaka za Ujerumani kwa taifa hilo la kifalme kaskazini mwa Afrika, kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu. 

Chama cha Polisario kinachoungwa mkono na Algeria kinasaka uhuru wa jimbo la Sahara Magharibi, ambalo ni eneo kubwa la jangwani linaloshikiliwa na Morocco tangu kumalizika kwa ukoloni wa Uhispania  mwaka 1975, na ambalo serikali mjini Rabat inalichukuliwa kuwa jimbo lake la kusini.

Tangu kuanza kwa mzozo huo, mamilioni ya raia wa Sahara Magharibi wamekimbilia mataifa jirani, ikiwemo Algeria, ambako kuna kambi kubwa kabisa za wakimbizi, ambazo Umoja wa Mataifa unasema zimesahaulika na dunia. 

Baada ya tangazo la Marekani kuitambuwa Morocco kama yenye mamlaka kwa nchi yao, vijana wengi kwenye kambi za wakimbizi walinukuliwa na vyombo vya habari wakisema kwamba wanalazimika kurejea tena kwenye vita vya silaha na serikali mjini Rabbat kwa kuwa hawana matumaini ya kurejeshewa nchi yao kupitia mazungumzo.