1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morales aiomba UN na Papa Francis kusuluhisha mzozo Bolivia

15 Novemba 2019

Rais aliyejiuzulu Evo Morales hataweza kugombea  kwenye uchaguzi wowote mpya, kiongozi huyo wa zamani ametoa mwito kwa Umoja wa Mataifa ama Papa Francis kusuluhisha mzozo huo wa kisiasa unaoendelea kufukuta nchini humo.

https://p.dw.com/p/3T7uS
Mexiko Präsident Evo Morales
Picha: picture-alliance/Zumapress/El Universal

Wakati rais wa mpito wa Bolivia Jeanine Anez akisema rais aliyejiuzulu Evo Morales hataweza kugombea  kwenye uchaguzi wowote mpya, kiongozi huyo wa zamani ametoa mwito kwa Umoja wa Mataifa ama Papa Francis kusuluhisha mzozo huo wa kisiasa unaoendelea kufukuta nchini humo, huku akisema bado anajitambua kama rais wa Bolivia. 

15.11.2019 Taarifa ya habari asubuhi

Morales aliyeko uhamishoni nchini Mexico anadai kwamba bado ni rais wa taifa hilo kwa kuwa bunge la Bolivia bado halijakubaliana na uamuzi wake wa kujiuzulu.

Bolivia imejikuta katika hali geni hii leo, wakati wabunge wakijaribu kufikia makubaliano ya kufanyika uchaguzi mpya, huku kukiwa na maandamano katika baadhi ya maeneo nchini humo na upinzani dhidi ya kiongozi huyo aliyejitangaza rais.

Morales amesema kwenye mahojiano na shirika la habari la AP akiwa Mexico alikoomba hifadhi ya kisiasa, kwamba kama bunge la Bolivia halijaukubali ama kuukataa uamuzi wake wa kujiuzulu, hivyo bado anaamini kwamba yeye ni rais.

Bolivien Senatorin Jeanine Anez
Rais wa mpito Jeanine Anez amesema Morales hataweza kugombea tenaPicha: picture-alliance/dpa/J. Karita

Lakini katika hatua nyingine ameutolea mwito Umoja wa Mataifa ama kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kusuluhisha mzozo huo, kufuatia kile alichokitaja kuwa ni mapinduzi. Alisema Nina imani kubwa na Umoja wa Mataifa. Kwa sababu tumekwishakuwa na mazungumzo ya kina na katibu mkuu, ndugu yangu Antonio. Anatakiwa kuwa msuluhishi akiwa na taasisi hiyo na si tu msimamizi, na labda kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki, na iwapo Papa Francis atahitajika, tunatakiwa kumjumuisha."

Huko Bolivia hali si shwari hasa baada ya maelfu ya wafuasi wake kuingia mitaani wakishinikiza kiongozi huyo wa zamani kurejea Bolivia. Walisikika kwenye mji wa Sabaca wakipaza sauti "Evo, rafiki, watu wako upande wako!"

Wafuasi hao ambao usiku wa jana walitokea mitaa ya Chapare eneo ambako Morales alijipatia umaarufu kabla ya kuwa rais wa kwanza kutoka watu wa asili, walizuiwa na wanajeshi kuufikia mji wa Cochabamba, ambako wafuasi wa Morales na wale wa upinzani walipambana wiki kadhaa zilizopita.

Morales amelieleza shirika hilo la habari la AP kwamba atarejea Bolivia, ikiwa hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa suluhu la mzozo huo.

Mchambuzi wa kisiasa kutoka shirika moja lisilo la kifaida la Andean Information Network in Bolivia, aliyeishi nchini humo kwa karibu miaka 30 amesema, huenda Morales akawa na hoja. Amesema, barua ya kujiuzulu inatakiwa kuwasilishwa, kujadiliwa na kukubaliwa katika kikao cha pamoja kabla hatua hiyo haijaanza kutekelezwa.