1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bin Salman awasili katika Falme Za Kiarabu kwa ziara

23 Novemba 2018

Mohammed Bin Salman amewasili katika Falme za Kiarabu ikiwa ni kituo chake cha kwanza cha ziara yake katika mataifa mbalimbali ya Kiarabu. Hii ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu mauaji ya Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/38mMt
Saudi-Arabien - Saudischer Kronprinz Mohammed bin Salman
Picha: picture alliance/abaca/Balkis Press

Mohammed Bin Salman pia anatarajiwa kuhudhuria kwenye mkutano wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia za kundi la G20 utakaofanyika mjini Buenos Aires, nchini Argentina mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba.

Mkutano huo utahudhuriwa pia na viongozi wa Marekani, Uturuki na Ulaya. Ziara ya bin Salman katika nchi za kiarabu inajiri wakati Saudi Arabia ikizidi kushinikizwa kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi katika ofisi ya ubalozi mdogo wa Saudia tarehe 2 Oktoba mwaka huu.

Salman amekutana na Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed na kujadili maendeleo ya kimataifa na kikanda, pamoja na changamoto na vitisho vinavyolikabili eneo la Mashariki ya Kati. Msemaji wa Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan, amesema Rais huyo atakutana na bin Zayed wakati wa mkutano  wa G20.

Saudi Arabien - Türkei l Saudischer Kronprinz Mohammed bin Salman und der türkische Präsident Erdogan
Mohammed bin Salman na Rais wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AP Photo/Presidency Press Service

Mkutano huo ndio utakaokuwa wa kwanza kwa Mohammed bin Salman na Rais Erdogan kukutana ana kwa ana tangu mauaji ya Khashoggi, ambayo yameipa sura mbaya utawala wa Saudi Arabia pamoja na bin Salman mwenyewe. Jumatano tarehe 21, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Adel al-Jubeir alisema kashfa dhidi ya Mohammed bin Salman na kutaka awajibishwe kwa mauaji ya Khashoggi hayatavumiliwa.

Jana Alhamisi, Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini aliishinikiza waliohusika na mauaji ya Khashoggi wawajibishwe, na kutaka uchunguzi wa wazi na wa kuaminika ufanyike. Mogherini amesema,´´Tunatarajia kwamba waliohusika na mauaji hayo ya kikatili watawajibishwa. Katika Umoja wa Ulaya. kwetu sisi uwajibikaji haumaanishi kisasi. Tumekuwa, na nataka kusisitiza hili, tangu mwanzo tunaendelea kupinga hatua yoyote ya utumiaji wa adhabu ya kifo.Lakini tunatarajia, kulingana na kanuni na maadili yetu ya kuendesha mifumo ya kisheria, uchunguzi kamili, wa uwazi na haki utafanyika.´´

Belgien EU Gipfel in Brüssel Federica Mogherini
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya, Federica MogheriniPicha: picture-alliance/dpa/T. Roge

Wakati huo huo wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema itawawekea vikwazo raia 18 wa Saudi Arabia kufuatia mauaji ya Khashoggi. Kadhalika  Denmark ilisitisha mpango wa kuiuzia Saudi Arabia silaha, nchi ya pili kuchukua uamuzi huo baada ya Ujerumani.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf