1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi amuambia Putin afanye mazungumzo na Zelensky

22 Oktoba 2024

Rais Vladimir Putin wa Urusi anaendelea kuwapokea na kukutana na viongozi mbalimbali wa dunia walio tayari kwa ajili ya mkutano wa 16 wa kilele wa jumuiya ya BRICS ambao unafanyika mjini Kazan.

https://p.dw.com/p/4m6Ef
BRICS Putin Modi Kazan
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi (kushoto), akiwa na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin wa Urusi, wakati wa mkutano wa kilele wa BRICS.Picha: Alexander Zemlianichenko/Pool via REUTERS

Kufikia mchana wa Jumanne (Oktoba 22), tayari Rais Putin alishamkaribisha na kufanya mazungumzo ya pande mbili na Waziri Mkuu Narendra Modi wa India na Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini. 

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Rais Putin amesema uhusiano baina ya India na Urusi unazidi kuimarika kila uchao na kwamba kwa pamoja serikali za mataifa hayo zinao uwezo wa kuzikabili changamoto kwenye siasa za kilimwengu.

"Mahusiano ya Urusi na India yana tabia ya ushirikiano mkubwa wa kimkakati na yanaendelea kuimarika kwa kasi. Tunaupokea na kuukaribisha uamuzi wako wa kufungua Ofisi ya Ubalozi wa India mjini Kazan. Utanuzi wa nafasi ya kidiplomasia ya India nchini Urusi utachangia zaidi kwenye maendeleo ya pande zetu mbili." Alisema Putin.

Soma zaidi: Putin mwenyeji wa mkutano wa kilele wa BRICS

Kwa upande wake, Modi, ambaye hii ni mara ya pili kuizuru Urusi kwa nia ya kusaka makubaliano ya kusitisha vita vya Ukraine, alitumia fursa ya mazungumzo yake ya leo na Putin kurejelea msimamo wake huo.

BRICS I Putin Dilma Rousseff
Rais Vladimir Putin wa Urusi akimkaribisha mkuu wa Benki ya Maendeleo na rais wa zamani wa Brazil, Dilma Rousseff, kwenye mkutano wa kilele wa BRICS mjini Kazan, Urusi.Picha: Alexander Nemenov/Pool via REUTERS

"Kuhusiana na mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine, tumekuwa na mawasiliano ya kudumu baina yetu na tunaamini matatizo haya yanapaswa kumalizwa kwa njia ya amani. Tunaunga mkono kikamilifu hatua za kufikia amani na utangamano haraka iwezekanavyo. Kwenye juhudi zetu, tunaweka kipaumbele chetu kwenye ubinaadamu, na tuko tayari kutoa msaada wowote utaohitajika." Alisema Modi.

Modi aliitembelea Ukraine mnamo mwezi Agosti na alikuwa Urusi mwezi Julai mwaka huu kuzitaka pande hizo mbili zikae kwenye meza ya mazungumzo, huku India ikibeba jukumu la kuwa mpatanishi mkuu. 

Ramaphosa amsifia Putin kama rafiki wa kweli

Kwa upande wake, Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambaye nchi yake ni miongoni mwa waanzilishi wa jumuiya ya BRICS, alimuambia mwenyeji wake, Rais Putin, kwamba nchi yake inathamini sana kile alichokiita "mahusiano tunu" baina ya mataifa yao mawili. Rais huyo wa Afrika Kusini alisema Putin ni rafiki na mshirika wa kweli  kwa Afrika Kusini tangu zama za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

BRICS I Putin  Ramaphosa
Rais Vladimir Putin wa Urusi (mbele) akimpokea mgeni wake, Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini, mjini Kazan, kwa ajili ya mkutano wa kilele wa jumuiya ya BRICS.Picha: Sputnik/Mikhail Metzel/Pool via REUTERS

Rais Xi Jinping wa China, Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ni miongoni mwa viongozi wakubwa wa ulimwengu ambao wanahudhuria mkutano huu wa siku tatu wa jumuiya inayokuwa kwa kasi ya BRICS, ambayo inasaka kujitambulisha kama mbadala wa mfumo na madhubuti wa kimataifa kando ya ulimwengu unaotawaliwa na mataifa ya Magharibi.

Soma zaidi: Ukraine yamlaumu Guterres kukubali mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS

Mkutano huo ambao wengi wanasema unajenga taswira ya jinsi mataifa ya Magharibi yalivyoshindwa kwenye juhudi zao za kuitenga Urusi baada ya uvamizi wake dhidi Ukraine, unatarajiwa kupitisha maazimio muhimu sana juu ya ushirikiano wa kifedha utakaoukwepa mfumo unaotawaliwa na Marekani.