1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa WHO azidi kuwa ngangari licha ya ukosoaji

Ibrahim Swaibu
18 Mei 2020

Shirika la afya duniani WHO limekuwa katika mstari wa mbele kupambana na janga la Corona, lakini baadhi ya viongozi wamelishonyea vidole vya lawama shirika hilo kwa kuwa na upendeleo kwa baadhi ya mataifa.

https://p.dw.com/p/3cQfK
Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Getty Images/Afp/F. Coffrini

 Mkuu wa shirika hilo Tedros  Adhanom Ghebreyesus, mara kadha amekosolewa na rais Trump wa Marekani. Hatahivyo mkuu huyo anasisitiza kuwa yuko imara kuongoza juhudi dhidi ya COVID-19 huku wachambuzi wakisema shirika hilo na Tedros wanapaswa kuungwa mkono kwa jitihada zake dhidi ya COVID-19. 

Licha ya kuitwa kibaraka wa rais Xi Jinping wa  China, kushambuliwa kwa matamshi ya ubaguzi wa rangi  na kukejeliwa katika mitandao ya kijamii, Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkrugenzi mkuu wa shirika la afya duniani anazidi kujitahidi kujenga mshikamano wa kimatifa  dhidi ya janga la COVID 19. Janga  ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000 na kukwamisha shughuli za uchumi katika mataifa maskini na tajiri.

Wataalamu wengi wa afya duniani wamempongeza Tedros pamoja na WHO kwa jitihada zake tangu mripuko wa virusi vya Corona licha ya utawala wa rais Donald Trump wa Marekani kulikosoa shirika hilo la Umoja wa matiafa.

WHO-Chef Tedros Adhanom trifft Chinas Präsidenten Xi jinping
Tedros Adhanom akiwa ktika mkutano na rais wa Chin, Xi Jinping, Januari 28, 2020, mjini Beijing.Picha: Getty Images/Afp/N. Hatta

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa shirika hilo unatathmini utendaji kazi wa Tedros ambao mara hii utafanyika kwa njia ya mtandao. Baadhi ya wakosoaji wa Tedros na wachambuzi wanamulika historia yake kama waziri wa serikali nchini Ethiopia, taifa lenye historia ya tawala za kiimla.

Muda si mrefu baada ya kuingia madarakani mwaka 2017, Tedros alimteua rais wa Zimbabwe wakati huo, Robert Mugabe, ambaye alikuwa akisafiri mara kwa mara ng'ambo kutafuta matibabu, kama balozi wa hisani wa WHO, kabla ya kutengua uteuzi huo kufuatia wimbi la ukosoaji wa mitandaoni.

''Ukikosoa WHO ama Tedros, kwa kiasi fulani unatizamwa kama mfuasi wa utawala wa Trump na unapoliteteta shirika hilo au kumtetea Tedros, unaonekana kama mtu anaeunga mkono ushirikiano wa Tedros na madikteta na viongozi wa kiimla duniani'', anasema Jeffey Smith, mtaalamu wa masuala ya demokrasia kutoka shirika la Vanguard Afrika lenye makao yake mjini Washington.

Smith anasema kuwa hapana shaka Tedros amewahi kuhudumu katika serikali za kidikteta na mara nyingi ameonyesha uhusiano wake nao lakini anafanya kazi nzuri na yeye na WHO wanahitaji kuungwa mkono pamoja.

Tuhuma za kuipendelea China

Katika siku za hivi karibuni rais Donald Trump wa Marekani ameikosoa WHO kwa kuegemea zaidi China na kusifu kupita kiasi namna taifa hilo lilivyoshughulikia janga la Corona haswa akimlenga Tedros.

Schweiz | Pressekonferenz: Weltgesundheitsorganisation WHO - Ausbreitung des Coronavirus wird als Pandemie eingestuft
Tedros pamoja na wasaidizi wake katika WHO - Mkrugenzi wa masuala ya dharura ya kiafya Michael Ryan, na mkuu wa masual ya kiufundi Maria Van Kerkhove, katika moja ya mikutano ya taarifa kuhusu covid-19.Picha: Getty Images/AFP/F. Cofffrini

Hatahivyo Tedros amejiepusha kuyakosoa mataifa hayo mawili yenye nguvu zaidi ambayo ni wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na amewasifu marais wote wawili - Xi Jinping na Donald Trump, huku akiacha vidokezo vinavyoonekana kuelekezwa Beijing na Washington - alipotahadharisha hivi karibuni, dhidi ya kutumia virusi hivyo kama zana ya kisiasa.

Mkuu huyo amepuuza vitisho dhidi ya maisha yake na pia kusimama kidete kulitetea bara la Afrika. Ameikosoa serikali ya Taiwan, nchi isiyo mwanachama wa WHO kwa kile alichokiita kukubali matamshi ya ubaguzi dhidi yake.

Aliewahi kuwa balozi wa Marekani nchini Ethiopia katika miaka ya 1990, David Shinn amesema wakati Tedros akiwa waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia, alikuwa na ushirkiano mzuri na Beijing na Washington.

Hatahivyo Shinn alisema kuwa Tedros alichaguliwa kama mkuu wa WHO, katika kipindi ambacho nchi yake ilikuwa ikiegemea sana China kisiasa na kiuchumi.

Tedros, mtaaalmu wa ugonjwa wa Malaria alihudumu kama waziri wa afya na waziri wa mambo wa nje wa Ethiopia kabla ya kuchaguliwa katika nafasi yake ya sasa mwaka 2017, akiwa mtu wa kwanza kutoka barani Afrika kuongoza shirika la afya duniani.

Chanzo: AP