1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa WHO aonya dhidi ya 'utaifa wa chanjo'

Saleh Mwanamilongo
26 Oktoba 2020

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa katika uzinduzi wa chanjo,wakati idadi ya maambukizi ikiongezeka kote duniani. 

https://p.dw.com/p/3kRUZ
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Direktor WHO
Picha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/S. D. Nolfi

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa katika uzinduzi wa chanjo yoyote ya virusi vya corona katika siku za usoni, wakati idadi ya maambukizi ikiongezeka kote duniani. 

Katika hotuba ya video wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa Afya Duniani ulioandaliwa  mjini Berlin Jumapili jioni, Ghebreyesus alisema njia pekee ya kujikwamua kutokana na janga hilo ni kushirikiana na kuhakikisha kuwa nchi maskini zina fursa sawa ya kupata chanjo. Wanasayansi kote duniani wanapambana kutengeneza chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, ambao umewauwa zaidi ya watu milioni 1.1.

'' Ikiwa na wakati tutakapo kuwa na chanjo rasmi, tunapaswa kuitumia kikamilifu. Na njia muafaka ya kufanya hivyo ni kuwapa chanjo baadhi ya watu katika nchi zote na sio watu wote katika nchi kadhaa''

Miito ya mshikamano wa kimataifa dhidi ya Covid-19

Rais wa shirikisho la Ujerumani,Frank Walter Steinemeier  ambae ni mwenye kiti wa mkutano huo utakao dumu hadi Jumanne, ametoa mwito wa mshikamano wa kimataifa katika kupambana na wimbi hili la pili la janga la Covid-19 na kupinga kile alichoita kuwa ni utaifa kuhusu chanjo. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres na rais wa Halmashauri ya umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen pia walihotubia mkutano huo.

 Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza, Japani na mataifa mengine kadhaa tayari yameweka oda kubwa na makampuni yanayohusika na utengenezaji wa chanjo zinazoonekana kuwa bora. WHO imeripoti jana siku ya tatu mfululizo yenye maambukizi mengi kote duniani, na kuzitaka nchi kuchukua hatua zaidi ya kusambaa kwa ugonjwa huo. Zaidi ya visa 465,319 vimetangazwa Jumapili pekee, nusu ya idadi hiyo ikiwa barani Ulaya.

China Das Labor des chinesischen Impfstoffhersteller Sinovac Biotech in Peking
Picha: Thomas Peter/File Photo/Reuters

Wimbi la pili la Covid-19 barani Ulaya

Nchini Ufaransa, bodi ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19 imetangaza kwamba mnamo siku za usoni wanatarajia kurikodi visa laki moja kwa siku.

Uhispania imetangaza hali ya kitaifa ya dharura ili kupambana na wimbi la pili la virusi vya corona. Wakati ugonjwa huo ukiendelea kuenea kwa kasi Ulaya, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez pia alitangaza amri ya kutotembea nje usiku kote nchini humo isipokuwa kuwa tu katika Visiwa vya Canary.

 Italia ,ambayo ilikuwa kitovu cha mripuko wa kwanza Ulaya , pia iliimarisha vizuizi vya maisha ya kila siku, kwa kuamuru kufungwa kumbi za sinema na mazoezi pamoja na mabaa na migahawa. Waandamanaji kadhaa wa misimamo mikali mjini Rome walikabiliana na polisi ya kuzuia ghasia usiku kucha wakati wa maandamano ya kupinga amri ya kutotembea nje. Polisi mjini Berlin pia waliyavunja maandamano ya kupinga vizuizi vya corona, na kuanzisha uchunguzi baada ya jengo lenye ofisi za shirika la afya ya umma kushambuliwa kwa moto.

 Viongozi wa Urusi waliripoti  leo Jumatatu visa vipya 17,347 mnamo masaa 24, vikiwemo vifo visa 5,224 mjini Moscow pekee. Urusi hivi sasa inajumla ya visa zaidi ya milioni 1.5.