1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

Mkuu wa UN atoa wito wa kuwasaidia Warohingya

17 Oktoba 2023

Mkuu wa Shirika la kushughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filippo Grandi, ameihimiza jumuiya ya kimataifa kutosahau masaibu yanayaowakabili wakimbizi wa Rohingya kutoka Myanmar.

https://p.dw.com/p/4XeWG
Schweiz | PK Filippo Grandi
Mkuu wa Shirika la kushughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR ,Filippo Grandi.Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Usaidizi zaidi unahitajika kuwasaidia Warohingya waliofurushwa na pia kupunguza mzigo kwa nchi zinazowakaribisha. 

Grandi amesema upatikanaji wa misaada ya kibinadamu unazidi kuwa mgumu kutokana na kuongozeka kwa migogoro  ya kivita nchini Myanmar na kupunguzwa kwa ufadhili na misaada kutokana na majanga mengine katika mataifa mbalimbali kama vile Afghanistan, Ukraine na Mashariki ya Kati.

Soma pia: UNHCR yahofia kutekelezwa wakimbizi wa Rohingya

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa kikanda kuhusu msaada wa wakimbizi wa Rohingya mjini Bangkok, Grandi amesisitiza kuwa suluhisho wanalohitaji zaidi wakimbizi wa Rohingya ni kile alichokitaja kama "kurudi kwa hiari na heshima nchini Myanmar "  lakini amekiri kwamba kuna "changamoto nyingi ambazo zinahitaji kushughulikiwa."

Aidha Grandi amewaomba washiriki katika mkutano huo kuweka ahadi za kuunga mkono wakimbizi wa Rohingya, kuweka sera wazi kwa nchi zilizowapokea wakimbizi hao, kutoa michango kwa nchi wafadhili na  umakini kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

"Lakini ni muhimu katika ulimwengu huu wenye matatizo na matatizo ambayo tunaishi tusisahau majanga yaliyopo, vinginevyo kwa bahati mbaya watu ambao wameathiriwa na mgogoro huu, Warohigya na nchi zinazowakaribisha zitapitia wakati mgumu kwasababu ya migogoro mengine." Alisema Grandi.

Hii leo Uingereza imetangaza msaada wa pauni milioni 4.5 za mahitaji ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh.

Mgogoro wa wakimbizi Myanmar

Indien Unterricht für Rohingya Kinder in Faridabad bei Neu Delhi
Watoto katika kambi ya wakimbizi ya Warohigya huko Faridabad, India.Picha: Nidhi Suresh/DW

Ziadi ya wakimbizi milioni moja wa Rohingya wamekimba Myanmar na kwenda Bangladesh kwa miongo kadhaa, ikijumuisha wengine takriban 740,000 waliovuka mpaka kuanzia Agosti 2017, wakati jeshi la Myanmar lilipoanzisha operesheni ya kikatili ya kukabiliana na mashambulizi yanayofanywa na makundi ya wapiganaji wa msituni.

Mwaka jana Marekani ilisema kwamba ukandamizaji ulifanywa dhidi ya Warohingya nchini Myanmar ni sawa na mauaji ya halaiki, hii ni baada ya maafisa wa Marekani kuthibitisha matukio ya ukatili dhidi ya raia unaofanywa na wanajeshi katika kampeni ya kimfumo dhidi ya makabila madogo.

 soma pia: Warohingya Bangladesh huenda wakakabiliwa na utapiamlo

Warohingya, ambao ni Waislamu, wanakabiliwa na ubaguzi katika nchi hiyo ambayo walio wengi ni waumini wa imani ya  Budha, huku wengi wakinyimwa uraia na haki nyingine nyingi.

Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe kutoka Bangladesh, Uingereza, India, Indonesia, Malaysia, Thailand na Marekani pamoja na  wawakilishi wa mashirika yanayoongozwa na Warohingya. Lakini kulingana na msemaji wa Umoja wa Mataifa Babar Baloch, hakukuwa na mwakilishi yeyote kutoka Myanmar.

Myanmar na Bangladesh zilikubali mchakato wa kuwarejesha makwao wakimbizi wa Rohingya katika muda wa miaka miwili mnamo mwaka 2018, Lakini usalama nchini Myanmar umezidi kuwa mbaya kufuatia jeshi kuchukua zaidi ya miaka miwili iliyopita ambayo iliiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa ya Aung Sun Suu Kyi, kuchochea upinzani mkubwa wa silaha, na mipango ya kuwarejesha makwao wakimbizi hao haijafaulu.