Mkuu wa polisi Tanzania aahidi uchaguzi wa amani
16 Oktoba 2020Amesema katika baadhi ya maeneo ikiwamo lile la Tarime mkoani Mara kuna wanasiasa wanaoandaa makundi ya vijana kwa lengo hilo hilo la kutaka kuona kwamba uchaguzi huo hauendi salama.
ila kuwataja wanasiasa hao au makundi hayo ya vijana, IGP Sirro amesema jeshi lake linawafahamu fika wale wote walioko nyuma ya vitendo hivyo na ameonya kwamba watashughulikiwa hata kabla ya uchaguzi wenyewe utakaofanyika Oktoba 28.
Amesema makundi hayo yanawahusisha pia vijana kutoka nchi jirani ambao wanaandaliwa kwenda kufanya fujo katika baadhi ya maeneo ili kutibua shughuli za uchaguzi
Mbali ya kutoa onyo kwa makundi hayo IGP Sirro ameeleza jinsi jeshi hilo lilivyo tayari katika kuelekea uchaguzi mkuu akisema limejipanga kukabiliana na hali yoyote ya ukorofi inayoweza kujitokeza.
Jeshi hilo ambalo wakati mwingine limekuwa likitupiwa lawama na baadhi ya vyama vya upinzani limepanga kusambaza askari wake katika maeneo yote ya uchaguzi, na IGP Sirro anasema kwenye maeneo ambayo yanatiliwa shaka kiwango cha askari watakaosambazwa kitaongezwa mara dufu.
Katika hatua nyingine, balozi wa Marekani nchini, Dr Donald Wright amemaliza kukutana na viongozi wote wa vyama vya siasa ikiwamo wagombea kujadiliana kuhusu masuala ya uchaguzi mkuu.
Amekuwa akikutana nao kwa nyakati tofauti na katika mazungumzo yake amekuwa akielezea matarajio ya Marekani kwenye uchaguzi huu ambao ni kuona unaendeshwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na uwazi.
Chama cha mwisho kukutana nacho na kufanya mazungumzo hayo ni chama tawala CCM, kilichowakilishwa na katibu wake mkuu, Dr Bashiru Ally, ambaye ameelezea kiini cha mazungumzo yao na mwanadiplomasia huyo aliyewasili nchini miezi miwili iliyopita.
Tanzania imewafungulia milango waangalizi wa kimataifa kuja kufuatilia uchaguzi huu na tayari mataifa kadhaa ya magharibi pamoja na taasisi nyingine za kimataifa zimeelezea utayari wao kuwasili nchini kwa jambo hilo.
Mwandishi: George Njogopa/DW-Dar es Salaam