1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Kanisa Katoliki Kongo ahimiza utulivu

25 Desemba 2023

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Kinshasa, Kadinali Fridolin Ambongo, ametoa wito wa kujizuia kufuatia kile alichokielezea kuwa "machafuko makubwa" ya uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4aYpc
DR Kongo | Kadinali Fridolin Ambongo
Kadinali Fridolin Ambongo amehimiza amani na kuwataka watu wajiepushe na vurugu za uchaguzi.Picha: Giscard Kusema/Presse- und Kommunikationsdienst der Präsidentschaft von Kongo

Ametoa wito huo usiku wa kuamkia leo wakati wa Misa yake ya Krismasi.

Ameongeza kuwa wengi walijitokeza kwa shauku na kwa dhamira ya kufanya maamuzi ya kidemokrasia, lakini kile ambacho kilipaswa kuwa sherehe kubwa ya maadili ya kidemokrasia, kiligeuka kuwa fadhaa kwa wengi.

Soma pia: Kanisa Katoliki Kongo lamshutumu Tshisekedi

Ucheleweshaji mkubwa wa vifaa na matatizo ya hapa na pale yaliathiri uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumatano iliyopita katika baadhi ya vituo.

Wagombea watano wa urais kutoka upinzani, akiwemo Moise Katumbi, wametaka uchaguzi huo ubatilishwe na kufanywa upya, wakisema ulikumbwa na "udanganyifu mkubwa".