Mkutano wa UN wamalizika kwa makubaliano ya kuiunga mkono UN
2 Oktoba 2018Mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa umemalizika huku rais wa baraza kuu la Umoja huo Maria Fernanda Espinosa akisema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni dunia kuunga mkono Umoja wa Mataifa pamoja na kutilia mkazo juu ya ushirikiano wa pamoja kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Rais wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa alisema wakati wa mjadala katika mkutano huo uliochukua wiki moja mjini New York viongozi wa dunia walitoa ujumbe wa pamoja juu ya haja ya kuunga mkono hoja ya ushirikiano wa pamoja.
Ameongeza kuwa inaleta usumbufu wakati baadhi ya nchi zinapoamua kujitoa katika wajibu wa kimataifa huku akiongeza kuwa hata hivyo dunia inalazimika kuheshimu tofauti hizo zilizopo.
Viongozi kadhaa walionekana kukosoa kauli ya rais Donald Trump wa Marekani aliyoitoa wakati akilihutubia baraza hilo la Umoja wa Mataifa ambapo alizipinga nadharia za utandawazi na kusisitiza kuunga mkono misimamo ya kizalendo.
Tangu rais Trump ashike madaraka Marekani tayari imejitoa katika makubaliano kadhaa ya kimataifa ikiwa ni pamoja na makubaliano ya nyukilia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani pamoja na mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi uliosainiwa mjini Paris.
Utawala wa rais Donald Trump tayari pia umejitoa katika makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji yanayotarajiwa kuidhinishwa mwezi Desemba nchini Morocco.
Suala la mabadiliko ya tabia ya nchi, kuzuia migogoro pamoja na suala linalohusu ushirikiano wa pamoja kimataifa yalikuwa ni miongoni mwa masuala yaliyogusiwa na wazungumzaji wengi katika mkutano huo wakiwemo wakuu wa mataifa 77, makamu wa rais kutoka mataifa matano na viongozi 44 wa serikali.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliifungua mkutano huo leo akisema ulimwengu hivi sasa una matumaini makubwa katika ushirikiano na kuonya kuwa ushirikiano huo unaonekana kupigwa vita katika wakati ambao unahitajika zaidi.
Miongoni mwa nchi chache zilizozungumzia juu ya utaifa ni Hungary ambayo ilijenga waya wa Sen'genge ili kuzuia wahamiaji .
Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Peter Szijjarto alisema uhamiaji ni changamoto na kuwa wimbi la wahamiaji linasababisha changamoto kubwa kiusalama na pia linaleta ugaidi katika maeneo ambayo hayajawahi kuwa na historia ya matukio ya kigaidi.
Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman